China yaweka vipaumbele vya maendeleo ya vijijini kwa Mwaka 2022

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 27, 2021
China yaweka vipaumbele vya maendeleo ya vijijini kwa Mwaka 2022
Picha iliyopigwa Septemba 23, 2021 ikionesha wakulima wakivuna mpunga katika Kijiji cha Hongguang, mji wa Changchun, Mkoa wa Jilin, Kaskazini-Mashariki mwa China. (Xinhua/Zhang Nan)

BEIJING - China imeweka vipaumbele vyake vya Mwaka 2022 katika maendeleo ya vijijini, na kuahidi hatua madhubuti na juhudi kubwa za kuunganisha kilimo na kuendeleza ustawishaji wa vijijini huku kukiwa na changamoto mbeleni.

Mkutano mkuu wa kila mwaka wa kazi za vijijini, uliofanyika kuanzia Jumamosi hadi Jumapili ya wiki iliyopita hapa Beijing, ulichambua hali ya sasa na kazi zinazokabili masuala yanayohusiana na kilimo, maeneo ya vijijini na wakulima na kuweka mpango wa mwaka ujao.

Rais Xi Jinping wa China, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi, ameongoza kikao cha Kamati ya Kudumu ya Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya CPC kuhusu masuala yanayohusu kilimo, maeneo ya vijijini na wakulima, na kuhutubia mkutano huo wa siku mbili.

Kilimo ikiwa sekta muhimu

Ikizingatiwa Mkutano Mkuu wa 20 wa CPC utakaofanyika Mwaka 2022, mkutano huo umesisitiza umuhimu maalum wa kuendeleza kazi za vijijini kwa hatua madhubuti ili kuweka mazingira kwa kuendeleza uchumi kwa utulivu na afya, kustawisha taifa na kuwafanya watu waishi kwa furaha na kufanya kazi kwa utulivu.

Rais Xi amesisitiza kuhakikisha maendeleo thabiti ya kilimo na maeneo ya vijijini wakati wa kukabiliana na hatari na changamoto nyingi.

Kuhakikisha usambazaji wa bidhaa za msingi ni suala kuu la kimkakati, Xi amesema, akitoa wito wa kufanya juhudi katika kulinda usalama wa nafaka na kulinda mashamba, kufanya marekebisho ya kimuundo ya ardhi, kupanua upandaji wa mazao ya soya na ya mafuta, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa nyama ya nguruwe, mboga mboga na bidhaa nyingine za kilimo na zile zinazotokana na kilimo.

Waziri Mkuu Li Keqiang, ambaye pia ni mjumbe wa kudumu wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya CPC, katika Mkutano Mkuu wa Baraza la Serikali, amesisitiza juhudi za kuhakikisha usambazaji wa rasilimali za uzalishaji wa kilimo, kuleta utulivu wa bei ya vyakula na kuhakikisha mavuno makubwa ya msimu wa joto.

Mwaka 2021, uzalishaji wa jumla wa nafaka wa China umefikia karibu kilo bilioni 683, ikiwa ni zaidi ya kilo bilioni 13.4 kutoka mwaka jana wa 2020, ambao ni mwaka wa saba mfululizo ambapo jumla ya uzalishaji wa nafaka nchini humo ulizidi kilo bilioni 650.

Mkutano huo umesema kuwa uzalishaji wa nafaka kwa Mwaka 2022 unapaswa kuwa zaidi ya kilo bilioni 650, wakati uzalishaji wa nguruwe unapaswa kuwa imara na utoaji wa mifugo, kuku, mazao ya majini na mboga unapaswa kutosheleza.

Kuhimiza ustawishaji vijijini

Katika kipindi cha miaka minane iliyopita, China imewaondoa wakazi wa mwisho maskini wa vijijini wapatao milioni 98.99 kutoka katika umaskini na kuondoa kata zote maskini 832 na vijiji 128,000 kutoka kwenye orodha ya umaskini.

Xi amesisitiza juhudi za kuhakikisha hakuna kiwango kikubwa cha watu kurudi kwenye umaskini, na kulinda na kuimarisha mafanikio ya China ya kupambana na umaskini.

Mkutano huo pia ulijadili rasimu ya waraka juu ya kuendeleza kazi kuu za ustawishaji wa vijijini mwaka ujao. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha