Watoto zaidi ya Milioni 8 Wenye Umri wa Chini ya Miaka 5 kuchanjwa Chanjo dhidi ya Polio huko Uganda

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 14, 2022
Watoto zaidi ya Milioni 8 Wenye Umri wa  Chini ya Miaka 5 kuchanjwa Chanjo dhidi ya Polio huko Uganda
Mtoto akidungwa chanjo kwenye kampeni ya kinga dhidi ya polio katika Kituo cha Afya huko Mtaa wa Wakiso, Uganda, Januari 13, 2022. Uganda imezindua kampeni ya udungaji chanjo dhidi ya polio kwa familia zote Alhamisi ya wiki hii. (Xinhua/Nicholas Kajoba)

Wizara ya Afya ya Uganda Jumatatu ya wiki hii ilisema, itawadunga chanjo dhidi ya polio watoto zaidi ya milioni 8 wenye umri wa chini ya miaka 5.

Ofisa mwandamizi wa shughuli za kinga na chanjo wa Wizara ya Afya ya Uganda Immaculate Ampeire alipohojiwa na Shirika la Habari la China, Xinhua alisema, zoezi la udungaji wa chanjo litafanywa nyumba kwa nyumba nchini kote kuanzia leo Januari 14 hadi 16.

Alisema, viongozi vya mabunge ya mitaani, timu za afya za vijiji, na maofisa wa afya watadunga chanjo hizo nyumba kwa nyumba.

Ampeire alisema, watoto milioni 8.8 hivi wenye umri wa chini ya miaka 5 watatumia chanjo mpya ya kumeza matone dhidi ya polio (nOPV2).

Agosti mwaka jana, baada ya kugundua virusi vya polio kwenye sampuli ya kinyesi iliyochukuliwa huko Kampala, Mji Mkuu wa Uganda, nchi hiyo ilitangaza mlipuko wa maambukizi ya Polio. Wizara ya Afya ilionya kuwa, virusi hivyo ni vya aina ya 2 isiyo kawaida, ambavyo chanjo dhidi yake iliondolewa kutoka shughuli za kawaida za udungaji za nchi hiyo Mwaka 2016.

Wizara ya Afya ya Uganda ilisema, virusi vya aina hiyo ni hatari zaidi katika aina zote za virusi vya polio. Kuibuka kwa virusi vya aina hiyo kumesababishwa na kupungua kwa udungaji wa kawaida wa chanjo katika nchi hiyo kutokana na maambukizi ya virusi vya korona.

Uganda ilitambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa nchi isiyo na Polio Oktoba, 2006 baada ya miaka 10 ya kutogunduliwa kwa visa vya Polio ndani ya nchi. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha