Njia mpya ya maji, sera ya masoko vyachangia kuongezeka kwa mapato ya Mfereji wa Suez wa Misri

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 14, 2022
Njia mpya ya maji, sera ya masoko vyachangia kuongezeka kwa mapato ya Mfereji wa Suez wa Misri
Picha iliyopigwa Machi 29, 2021 ikionesha meli ya makontena ya Ever Given ikielea katika maji kwenye Mfereji wa Suez, Misri. (Xinhua/Wu Huiwo)

CAIRO – Wataalam wa uchumi wa Misri wamesema kuwa, Mfereji wa Suez wa Misri ulifanikiwa kupata mapato ya juu zaidi ya kila mwaka katika historia yake Mwaka 2021 kutokana na njia mpya ya maji inayoenda sambamba na ile ya awali na sera ya masoko inayotekelezwa na Mamlaka ya Mfereji wa Suez (SCA) ili kuondokana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na UVIKO-19.

Mapema mwezi huu wa Januari, Mwenyekiti wa SCA Osama Rabie alisema mapato ya mfereji huo uliochimbwa na Serikali yalifikia dola za Marekani bilioni 6.3 Mwaka 2021, ikiwa ni ongezeko la asilimia 12.8 kuliko mwaka uliopita, ambayo ni ya juu zaidi katika historia ya mfereji huo.

Amebainisha kuwa njia ya maji pia ilipitisha tani kubwa zaidi za mzigo kila mwaka zipatazo bilioni 1.27 Mwaka 2021, ikilinganishwa na tani bilioni 1.17 Mwaka 2020, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 8.5.

Mohamed Ali Ibrahim, profesa wa Usafiri na Lojistiki katika Chuo cha Kiarabu cha Sayansi, Teknolojia na Usafiri wa Baharini, amehusisha ongezeko hilo ambalo halijawahi kushuhudiwa na ujenzi wa Mfereji mpya wa Suez, njia ya maji yenye urefu wa kilomita 35 iliyozinduliwa Mwaka 2015 pamoja na ile ya awali ya kilomita 190.

"Mfereji mpya umepunguza muda wa kusafiri kwa meli na kuvutia aina mpya za meli na kontena ambazo haziwezi kusafiri kupitia mfereji wa asili," profesa amesema.

Kwa mujibu wa SCA, idadi ya meli zilizopita pande zote mbili za mfereji Mwaka 2021 iliongezeka kwa asilimia 10 hadi 20,694, ikilinganishwa na ile ya 18,830 ya Mwaka 2020.

Mtaalam wa uchumi wa Misri Karim Al-Omda ameunga mkono kauli kwamba mapato ya kila mwaka ya Mfereji wa Suez ambayo hayajawahi kushuhudiwa yametokana na sera makini ya masoko ya SCA, ambayo imesaidia kuvutia idadi kubwa ya meli zilizokuwa zikisafiri kupitia njia nyingine za baharini.

"Upanuzi wa mara kwa mara unaotekelezwa na Serikali ya Misri kwenye Mfereji wa Suez umefanya mfereji huo kuwa na uwezo zaidi wa kupokea meli kubwa," ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.

Mfereji wa Suez ni njia kuu ya biashara ya baharini duniani kwani unapitisha meli zinazosafiri kati ya Ulaya na Asia Kusini bila kulazimika kuzunguka Bara la Afrika, na hivyo kupunguza umbali wa safari ya baharini kati ya Ulaya na India kwa takriban kilomita 7,000.

Kila mwaka, karibu asilimia 12 ya thamani ya biashara ya kimataifa, ikiwa ni sawa na zaidi ya asilimia 25 ya usafirishaji wa makontena duniani, hupitia Mfereji wa Suez. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha