

Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping aagiza kufanya uchunguzi kufuatia Ndege iliyobeba watu 132 kuanguka Kusini mwa China
BEIJING na NANNING - Rais Xi Jinping wa China ameagiza kufanya juhudi za utafutaji na uokozi za kila namna baada ya ndege ya abiria iliyokuwa na watu 132 kuanguka katika Mkoa unaojiendesha wa kabila la wazhuang wa Guangxi, China Jumatatu alasiri wiki hii.
Rais Xi amesema katika maagizo yake kwamba ameshtushwa na ajali ya ndege ya Shirika la Ndege la China Eastern Airlines ya namba MU5735.
Xi ameagiza hatua za haraka zichukuliwe kubaini chanzo cha ajali hiyo na kuimarisha maboresho ya usalama wa sekta ya usafiri wa ndege ili kuhakikisha usalama kamili wa sekta hiyo na maisha ya watu.
Naye Waziri Mkuu wa China Li Keqiang, pia amehimiza juhudi za kuzifariji familia za waathiriwa na kuwapa msaada, kutoa habari sahihi kwa wakati, kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo, na kuchukua hatua kali za kuimarisha usalama wa usafiri wa ndege.
Jana Jumatatu alasiri Idara ya Usimamizi wa Dharura ya Mkoa wa Guangxi ilisema, ndege ya abiria iliyokuwa na watu 132 ilianguka mkoani Guangxi, Kusini mwa China.
Idara hiyo ilieleza kuwa, ndege hiyo ya Shirika la Ndege la China Eastern Airlines aina ya Boeing 737, iliyokuwa ikitoka Kunming na kuelekea Guangzhou, ilianguka katika eneo la milimani karibu na Kijiji cha Molang cha Wilaya ya Tengxian katika Mji wa Wuzhou saa 2:38 usiku na kusababisha kulipuka kwa moto mlimani.
"Nilisikia mngurumo wa ndege upande wa pili wa mlima. Sekunde moja baadaye, kulikuwa na mlipuko," mfanyakazi karibu na eneo la ajali ameliambia Shirika la Habari la Xinhua, China.
Idara ya Usafiri wa Ndege ya Abiria ya China ilisema kwenye tovuti yake kwamba, ndege hiyo ya Namba MU5735 ilikuwa na abiria 123 na wahudumu tisa. Serikali imeanza kutekeleza utaratibu wa kukabiliana na hali ya dharura, na kikundi cha kazi kimewasili Wuzhou.
“Moto kutoka kwenye ajali hiyo umezimwa na shughuli ya uokozi inaendelea” amesema Chen Jie, ofisa kutoka idara ya usimamizi wa dharura ya mkoa huo.
Tayari Mkoa wa Guangxi na Mkoa jirani wa Guangdong imetuma vikosi kazi mbalimbali vikiwemo vya zima moto, wahudumu wa matibabu na wataalamu wa kisaikolojia kwende eneo la ajali ya ndege.
"Kuna mabaki ya ndege kwenye pengo mlimani," mfanyakazi wa uokozi katika eneo la ajali alimwambia mwandishi wa habari wa Xinhua. "Kuna vipande vya mbawa, kimoja kikiwa na urefu wa mita 2 au 3. Kuna uchafu mwingine, na pengine waweza kuwa vipande vya nguo."
Shirika la Ndege la Eastern Airlines la China limesema chanzo cha ajali hiyo kitachunguzwa kikamilifu.
Kampuni ya Boeing China, ambayo ni mtengenezaji wa ndege hiyo imesema imepata habari mbalimbali kutoka vyombo vya habari kuhusu ajali hiyo na inajitahidi kukusanya habari zaidi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma