

Lugha Nyingine
WTO yasema mgogoro wa Ukraine unaweza kupunguza kwa nusu ukuaji wa biashara duniani Mwaka 2022
GENEVA - Mgogoro unaoendelea kati ya Russia na Ukraine umeleta pigo kubwa kwa uchumi wa Dunia, ukipunguza makadirio ya ukuaji wa biashara duniani kwa Mwaka 2022 kutoka asilimia 4.7 iliyokadiriwa Mwezi Oktoba mwaka jana hadi kati ya asilimia 2.4 na asilimia 3.
Makadirio hayo, kwa kuzingatia mfumo wa ufuatiliaji wa uchumi wa Dunia, yalifanywa na Sekretarieti ya Shirika la Biashara Duniani (WTO) katika ripoti yake iliyotolewa Jumatatu wiki hii.
Kwa mujibu wa mfumo huo huo, mgogoro wa Ukraine unaweza kupunguza ukuaji wa Pato la Dunia (GDP) kwa asilimia 0.7-1.3, na kulifanya likue kati ya asilimia 3.1 na 3.7 kwa Mwaka 2022.
“Mgogoro huo umeongeza bei ya chakula na nishati, na kupunguza upatikanaji wa bidhaa zinazouzwa nje na Russia na Ukraine” ripoti ya Sekretarieti ya WTO inafafanua.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Russia na Ukraine zote ni wauzaji wakubwa wa bidhaa muhimu, haswa chakula na nishati. Nchi hizo mbili zilitoa takriban asilimia 25 ya ngano, asilimia 15 ya shayiri na asilimia 45 ya mauzo ya alizeti duniani kote Mwaka 2019. Russia pekee ilichangia asilimia 9.4 ya biashara ya nishati duniani, ikiwa ni pamoja na asilimia 20 ya mauzo ya gesi asilia.
“Russia ni moja ya wauzaji wakuu duniani wa palladium na rhodium, ambavyo ni muhimu katika utengenezaji wa magari. Wakati huo huo, uzalishaji wa semiconductor unategemea kwa kiasi kikubwa neon zinazotolewa na Ukraine. Kuvurugika kwa ugavi wa vifaa hivi kunaweza kuathiri uzalishaji wa magari wakati ambapo sekta hiyo inafufuka kutokana na uhaba wa semiconductor”, WTO imesisitiza.
Ulaya, soko kuu la bidhaa za Russia na Ukraine, ina uwezekano mkubwa wa kukumbwa na athari za kiuchumi. Kupungua kwa usafirishaji wa nafaka na vyakula vingine pia kutaongeza bei ya bidhaa za kilimo.
Ripoti hiyo ya WTO inasema Afrika na Mashariki ya Kati ndiyo maeneo yaliyo hatarini zaidi, kwa vile yanaagiza zaidi ya asilimia 50 ya mahitaji yao ya nafaka kutoka Ukraine na/au Russia. Kwa jumla, nchi 35 barani Afrika huagiza chakula na 22 huagiza mbolea kutoka Ukraine, Russia au zote mbili.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa, baadhi ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zinakabiliwa na uwezekano wa kupanda kwa bei ya ngano kwa asilimia 50-85, kutokana na athari za mgogoro katika usafirishaji wa nafaka.
"Mgogoro wa sasa unaweza kuzidisha hali ya ukosefu wa usalama wa chakula duniani wakati ambapo bei za vyakula tayari ziko juu kutokana na janga la UVIKO-19 na sababu zingine," inaonya WTO.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma