IMF yashusha makadirio ya ukuaji wa uchumi kwa nchi na maeneo zaidi 140 kutokana na mgogoro kati ya Russia na Ukraine

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 15, 2022
IMF yashusha makadirio ya ukuaji wa uchumi kwa nchi na maeneo zaidi 140 kutokana na mgogoro kati ya Russia na Ukraine
Kristalina Georgieva, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), akifanya mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua wakati wa Mikutano ya IMF ya majira ya mchipuko huko Washington D.C., Marekani, Aprili 13, 2021. (Kim Haughton/IMF/Kutolewa kupitia Xinhua)

WASHINGTON – Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) Kristalina Georgieva, Alhamisi wiki hii amesema kwamba shirika hilo litarekebisha makadirio yake ya ukuaji wa uchumi duniani kutokana na mgogoro kati ya Russia na Ukraine, ambao utachangia kushusha makadirio ya kukua kwa uchumi kwa nchi na maeneo 143 mwaka huu.

"Kusema kwa urahisi: tunakabiliwa na mgogoro juu ya janga," Bibi Kristalina Georgieva amesema kabla ya kufunguliwa kwa mikutano ya majira ya mchipuko kwa Mwaka 2022 ya IMF na Benki ya Dunia iliyopangwa kuanza wiki ijayo.

"Katika wiki saba zilizopita, Dunia imekumbwa na mgogoro mkubwa wa pili - vita juu ya janga. Hii inahatarisha kuzorotesha maendeleo mengi ambayo tumefanya katika miaka miwili iliyopita, ili kufufua kutoka janga la UVIKO," Georgieva amesema.

Katika ripoti yake mpya ya Mtazamo wa Uchumi Duniani (WEO) iliyotolewa Mwezi Januari mwaka huu, IMF tayari imepunguza makadirio ya kukua kwa uchumi Mwaka 2022 kwa asilimia 0.5 hadi asilimia 4.4 huku kukiwa na ongezeko la maambukizi ya virusi vya Korona hususan Omicron, na uchumi wa Dunia ukikabiliwa na matatizo ya usambazaji, mfumuko wa bei, madeni makubwa na hali ya kutokuwa na uhakika ya muda mrefu.

"Tangu wakati huo, mtazamo umezorota sana," kwa kiasi kikubwa kutokana na vita na athari zake," Georgieva amenukuliwa akisema.

Mkuu huyo wa IMF amebainisha kuwa athari za kiuchumi kutokana na mgogoro kati ya Russia na Ukraine zimeenea "haraka na mbali," "zikiwakumba sana watu walio hatarini zaidi duniani."

Amesema kwamba, msukosuko huo umeongeza bei ya nishati na chakula na kuzidisha mfumuko wa bei, na kuumiza mamia ya mamilioni ya familia ambazo tayari zilikuwa zinakabiliwa na kipato cha chini na bei ya juu, na kutishia kuongeza zaidi ukosefu wa usawa.

"Kwa hivyo, tunakadiria kuwa ongezeko la uchumi la mwaka 2022 na 2023 litashuka zaidi," Georgieva amesema, akibainisha kuwa athari za vita zitachangia kushuka kwa makadirio ya ongezeko la uchumi wa nchi na maeneo 143 mwaka huu – yanayochukua asilimia 86 ya Pato la Dunia (GDP). IMF itatoa Mtazamo wake wa Uchumi wa Dunia Jumanne wiki ijayo, Aprili 19.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi mkuu wa IMF, Vipaumbele vya haraka, ni kumaliza vita nchini Ukraine, kukabiliana na janga la UVIKO, na kukabiliana na mfumuko wa bei na madeni. Pia amesisitiza juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi, huku akiwataka watunga sera kukumbatia mageuzi ya kidijitali.

Ameshauri kwamba, ili kukabiliana na changamoto hizi, nchi zinapaswa kuwa tayari kutumia mbinu zote zilizopo, ambazo ni pamoja na kuongeza muda wa madeni na kutumia mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji fedha za kigeni na hatua za usimamizi wa mtaji.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha