Maendeleo ya kidijitali yasaidia watu zaidi nchini China kufurahia kusoma vitabu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 28, 2022
Maendeleo ya kidijitali yasaidia watu zaidi nchini China kufurahia kusoma vitabu
Ubao unaoonyesha njia mpya za usomaji vitabu kama ulivyopigwa picha wakati wa Mkutano wa Kwanza wa China wa Kusoma Vitabu uliofanyika Beijing, Mji Mkuu wa China, Aprili 23, 2022. (Xinhua/Luo Xin)

BEIJING - Cheng Zhiwu, mwenye umri wa miaka 70 kutoka Mkoa wa Hubei katikati mwa China, amepakua zaidi ya vitabu 600 vya kidijitali kwenye programu (APP) ya kusoma vitabu kwenye kompyuta yake ndogo.

"Nimepata furaha kubwa katika kusoma au kusikiliza vitabu vya kidijitali kama njia ya kwenda na wakati na kutajirisha miaka yangu ya dhahabu," anasema Cheng, huku akiongeza kuwa yeye hutumia saa nne hadi tano kwa siku kwenye programu hiyo ya kusoma vitabu.

Mkutano wa Kwanza wa China wa Kusoma vitabu umemalizika mjini Beijing siku ya Jumatatu wiki hii huku usomaji wa kidijitali ukifuatiliwa na watu wengi. Pamoja na maendeleo ya teknolojia na umaarufu wa mtandao wa simu, usomaji wa kidijitali umekuwa nguvu mpya ya kuhimiza watu wa rika zote nchini China kusoma vitabu.

Kwa mujibu wa ripoti kuhusu idadi ya wasomaji wa kidijitali wa China ya Mwaka 2021 iliyotolewa wakati wa mkutano huo, idadi ya wasomaji wa vitabu vya kidijitali nchini China ilifikia milioni 506 Mwaka 2021, ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.43 kuzidi mwaka 2020.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo sehemu kubwa iliandaliwa na Shirika la Uchapishaji wa Audio na Video Kidijitali la China, thamani ya jumla ya soko la usomaji wa kidijitali nchini China ilifikia yuan bilioni 41.57 (kama dola za kimarekani bilioni 6.3) mwaka jana, na ukuaji wake kwa ujumla ulifikia asilimia 18.23.

“Kama hali inayokua, usomaji wa sauti ulivutia zaidi ya watumiaji milioni 800 nchini China mwaka jana, ongezeko la watumiaji milioni 230 zaidi ya Mwaka 2020” anasema Fan Weiping, Mkuu wa Shirikisho la mashirika ya Redio na Televisheni ya China.

Inavyoonekana, usomaji wa sauti umekuwa kama daraja la kupunguza "pengo la kidijitali" kwa wasomaji wazee kama Cheng, na majukwaa kadhaa ya vitabu vya kielektroniki yamelenga kuboresha uzoefu wa usomaji wa sauti.

"Tunatoa orodha za vitabu lengwa kwa wasomaji wazee, na teknolojia ya akili bandia tunayotumia inaweza kubadilisha maandishi yaliyomo kuwa katika mfumo wa sauti kwa wasomaji wazee kila wanapohitaji kusikiliza” anasema Liu Xin, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Utamaduni ya Migu, wakati alipotambulisha toleo maalum la programu yao ya kusoma kwa wazee.

Bidhaa za China za usomaji wa kidijitali, haswa fasihi za mtandaoni, zimekuwa maarufu zaidi katika masoko ya ng'ambo. Zaidi ya vitabu 400,000 vya kidijitali kutoka China vilitolewa nje ya nchi mwaka jana. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha