

Lugha Nyingine
Raia wa China anayejitolea ang’arisha ndoto za watoto wanaoishi kwenye makazi duni nchini Kenya (4)
![]() |
Watoto wakipata chakula cha mchana bure shuleni katika eneo la makazi duni la Mathare, Nairobi, Kenya, Aprili 28, 2022.(Xinhua/Dong Jianghui) |
NAIROBI - Liu Yimenghan, kijana mchangamfu kutoka China, anasema uhusiano wake na makazi duni ya Mathare kwenye ukingo wa Mashariki wa Nairobi, Mji Mkuu wa Kenya, ulianza wakati alipoanza safari ya kujitolea katika miaka aliyokuwa akisoma chuoni katika eneo hilo na kisha kujitolea kuwa mwalimu wa somo la hisabati kwa mwaka mmoja na baadaye kuhisi moyo wa kuendelea na kazi yake hiyo ya hisani.
"Nilisoma somo la huduma kwa jamii katika chuo changu na nilikuwa nikishiriki kwenye shughuli za kutoa huduma ya kijamii huko Mathare. Na hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kufika Mathare na nilihisi kuwa labda kuna kitu ninaweza kufanya kupitia uwezo wangu," Liu mwenye umri wa miaka 27 anasema.
Liu aliwasili nchini Kenya akiwa na umri wa miaka 13, akisoma katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki hadi ngazi ya chuo kikuu, na kumpatia ufahamu wa kina wa jamii za wenyeji, utamaduni wao, imani na mifumo ya maadili. Kazi yake ya hisani imeng’arisha ndoto za watoto huko Mathare, eneo ambalo Liu anapendelea liitwe kwa jina la "makazi ya Mathare."
Liu ambaye ni mwanzilishi mwenza wa Asasi ya Huduma ya Kujenga Ndoto (DBSA), shirika lisilo la kiserikali lililoanzishwa Mwaka 2014, sasa anajivunia kuiona Mathare -- eneo la makazi duni la pili kwa ukubwa Nairobi – likibadilika kuwa makazi yake ya pili, licha ya umaskini uliokithiri, uhalifu na uchafuzi wa mazingira.
Anasema kwamba mara baada ya kuboresha hali ya madarasa kutoka madarasa yaliyojengwa kwa mabati chakavu hadi kukamililsha kuyajenga kwa matofali huko Mathare, kazi yake ya kujitolea ilibadilika na kuanza kujikita katika kutoa huduma ya chakula mashuleni, ufadhili wa masomo, ushauri na kukuza talanta kwa watoto wa Mathare.
Liu anasema kuwa ufadhili wa masomo hutolewa kila muhula na unalenga kuwahamasisha watoto kutoka katika mazingira duni na wazazi wao kuthamini elimu kwani ndiyo lango la mafanikio.
Shukrani kwa juhudi zake katika miaka minane iliyopita, shule tatu huko Mathare zimekarabatiwa, ambapo watoto maskini wanapata chakula cha mchana bila malipo na kupokea ufadhili wa masomo.
Akizungumza na Shirika la Habari la China, Xinhua wakati wa mahojiano ya hivi majuzi katika Kituo cha Masomo cha Mathare, moja ya shule tatu zilizokarabatiwa huko Mathare na DBSA, Liu anasema ushirikiano na mashirika ya misaada ya China na uchangishaji wa pesa mtandaoni umehakikisha uendelevu wa kazi ya hisani hapa.
Kevin Oluoch, naibu mwalimu mkuu wa Kituo cha Masomo cha Mathare amesema DBSA imekuwa ikitoa chakula bure cha kifungua kinywa na chakula cha mchana shuleni hapo tangu Mwaka 2017, akiongeza kuwa mpango wa kutoa lishe mashuleni umesaidia watoto kukua katika afya njema kwa sababu wanatoka katika familia zilizo hatarini ambazo haziwezi kumudu chakula cha mchana na kifungua kinywa.
Tangu Mwaka 2016, DBSA imekuwa ikifanya maonyesho ya vipaji, mechi za soka, maonyesho ya sanaa, mafunzo ya vijana na miradi mingine huko Mathare ili kuwasaidia watoto huko kutimiza ndoto zao.
Liu anasema baadhi ya shughuli hizi zimesitishwa kwa sababu ya janga la virusi vya Korona (UVIKO-19) na mpango wa kugawa lishe shuleni ndiyo kazi kuu ya hisani anayofanya kwa sasa.
Kwa mujibu wa Liu, miradi ya hisani ya DBSA inatekelezwa katika nchi sita barani Afrika, ambazo ni Kenya, Uganda, Tanzania, Ethiopia, Malawi na Nigeria, na mpango wa chakula pia kwa sasa unatekelezwa kwenye zaidi ya shule 40 katika nchi hizo sita.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma