Karibu vifo milioni 15 vinavyohusishwa na UVIKO-19 vimerekodiwa duniani kote

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 06, 2022
Karibu vifo milioni 15 vinavyohusishwa na UVIKO-19 vimerekodiwa duniani kote
Picha iliyopigwa Machi 30, 2021 ikionyesha mwonekano wa nje wa makao makuu ya Shirika la Afya Duniani (WHO) huko Geneva, Uswisi. (Xinhua/Chen Junxia)

GENEVA - Shirika la Afya Duniani(WHO) Alhamisi wiki hii limesema kwamba karibu vifo milioni 15 duniani kote vilivyotokea kufikia mwishoni wa Mwaka 2021 vinahusishwa moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na janga la virusi vya Korona (UVIKO-19).

Kwa mujibu wa makadirio ya WHO, idadi kamili ya waliofariki kutokana na UVIKO-19, au "vifo kupita kiasi," ilikuwa takriban milioni 14.9 kati ya Januari 1, 2020 na Desemba 31, 2021. Idadi hii inakokotolewa kwa kuzingatia tofauti kati ya idadi ya vifo ambavyo vimetokea na idadi ambayo ingekadiriwa kama janga hili lisingekuwepo kwa kuhusisha na takwimu kutoka miaka ya nyuma.

Ukiacha vifo vilivyosababishwa moja kwa moja na UVIKO-19, "vifo visivyo vya moja kwa moja" vilitokana na hali nyingine za kiafya ambazo watu hawakuweza kupata kinga na matibabu, kwa sababu mifumo ya afya ililemewa na janga hilo.

WHO imesema idadi kubwa ya vifo vilivyozidi -- asilimia 84 – vimeripotiwa zaidi Kusini-Mashariki mwa Asia, Ulaya na nchi za Mabara ya Amerika, na asilimia 68 katika nchi kumi tu duniani. Nchi za uchumi wa mapato ya kati zilichukua asilimia 81 ya vifo vya milioni 14.9, wakati nchi za uchumi wa mapato ya juu na chini zilichukua asilimia 15 na 4 .

Idadi ya vifo duniani ilikuwa kubwa zaidi kwa wanaume (asilimia 57) kuliko wanawake (asilimia 43) na ilikuwa kubwa zaidi miongoni mwa watu wazima wazee.

"Takwimu hizi muhimu siyo tu zinaonesha athari za janga hili lakini pia zinahitaji nchi zote kuwekeza katika mifumo thabiti zaidi ya afya ambayo inaweza kudumisha huduma muhimu za kiafya wakati wa majanga, pamoja na mifumo thabiti ya upashanaji wa habari kuhusu afya," Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema katika taarifa yake.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha