

Lugha Nyingine
Msaada wa Mradi wa miundombinu wa China waongeza nafasi ya Namibia katika usafirishaji (3)
WINDHOEK – Miradi ya msaada ya China inaendelea kusaidia maendeleo ya miundombinu nchini Namibia na mradi wa mpya wa hivi karibuni ukiwa ni uboreshaji wa Awamu ya 2B ya Barabara ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa kutoka Windhoek hadi Hosea Kutako.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Namibia, John Mutorwa amesema, mradi huo, ambao umewekwa jiwe la msingi jana Jumatatu huko Windhoek, Mji Mkuu wa Namibia, ni sehemu ya njia kuu za kikanda za Namibia na unajumuisha ujenzi wa barabara kuu ya njia mbili yenye urefu wa kilomita 21.3, njia tatu za makutano, madaraja mawili ya mito, na miundo ya mifereji ya maji.
“Namibia iko katika nafasi nzuri ya kuwa lango la uuzaji na uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwenda na kutoka kwa majirani wasio na bandari katika ukanda wa SADC (Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika) na China inatusaidia katika kupanua mtandao wetu wa barabara katika juhudi za kufikia dira na malengo ya usafiri kama ilivyoainishwa katika Dira ya 2030," amesema.
Mradi wa Awamu ya 2B unaofadhiliwa na serikali ya China unatarajiwa kuchukua miezi 36 kukamilika, amesema huku akiipongeza China kwa msaada wake mkubwa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Balozi wa China katika Ubalozi wa China nchini Namibia, Yang Jun, amesema mradi wa Awamu ya 2B ulipendekezwa na serikali ya Namibia na kuungwa mkono na ubalozi wa China katika juhudi za kusaidia Namibia kuwa kitovu cha usafirishaji Kusini mwa Afrika.
“Mradi huo ulithibitishwa rasmi na kutiwa saini kati ya serikali zetu mjini Beijing Machi 29, 2018,” amesema na kuongeza kuwa mradi utakapokamilika utaboresha usafiri na kuchangia maendeleo ya Namibia kwa ujumla.
Mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya Ukandarasi ya Zhong Mei kutoka China iliyosajiliwa nchini Namibia, pamoja na wakandarasi wadogo wa ndani, utatengeneza fursa za ajira zaidi ya 300 na kuchangia maendeleo ya kiteknolojia kupitia uhamishaji wa ujuzi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma