Barabara Kuu iliyojengwa kwa msaada wa China yaanza majaribio Nairobi, Kenya na kuleta uhai kwenye ukuaji wa uchumi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 16, 2022
Barabara Kuu iliyojengwa kwa msaada wa China yaanza majaribio Nairobi, Kenya na kuleta uhai kwenye ukuaji wa uchumi
James Macharia (wa tatu kushoto), Waziri wa Uchukuzi, Miundombinu, Nyumba na Maendeleo ya Miji wa Kenya, na wajumbe wengine wakipongeza majaribio ya matumizi ya barabara kuu ya Nairobi, Kenya, Mei 14, 2022. Kenya Jumamosi mwishoni mwa wiki ilianza matumizi ya majaribio ya barabara kuu ya Nairobi iliyojengwa kwa msaada wa China kabla ya kuanza kutumika rasmi katika wiki chache zijazo. (Picha na Fred Mutune/Xinhua)

NAIROBI - Kenya siku ya Jumamosi mwishoni mwa wiki ilianza majaribio ya matumizi ya barabara kuu ya Nairobi iliyojengwa kwa msaada wa China kabla ya kuanza kutumika rasmi wiki chache zijazo.

James Macharia, Waziri wa Uchukuzi, Miundombinu, Nyumba na Maendeleo ya Miji wa Kenya, amesema wakati wa mkutano na wanahabari huko Nairobi, Kenya, kwamba kuna shauku kubwa miongoni mwa madereva kutumia barabara hiyo ya kutoza ushuru inayoanzia upande wa Magharibi hadi kwenye ukingo wa Kusini-Mashariki wa mji mkuu huo.

"Ni moja ya miundombinu bora zaidi kuwahi kufanywa barani Afrika. Kwa hakika, ndiyo barabara kuu ndefu zaidi barani Afrika. Kwa hivyo, tunajivunia sana leo kuja kushuhudia kuanza kwa matumizi ya majaribio, ambayo yatafanyika kwa takriban wiki tatu au nne,” amesema Macharia, akiongeza kuwa watumiaji wa barabara 11,000 wa Kenya wamejiandikisha, na idadi itaongezeka hadi karibu 50,000.

Barabara Kuu ya Nairobi yenye urefu wa kilomita 27.1 inafadhiliwa na kujengwa na Kampuni ya Ukandarasi wa Barabara na Madaraja ya China chini ya mfumo wa ushirikiano wa sekta ya umma na sekta binafsi. Ujenzi kamili wa mradi huo unaogharimu takriban dola milioni 600 za kimarekani ulianza Septemba 2020.

Macharia amesema barabara hiyo kuu kwa muda uliovunja rekodi kwa sababu imekamilika mwaka mmoja kabla ya muda uliopangwa, na matokeo yake yatachangia maendeleo ya uchumi. Amebainisha kuwa mradi huo unawakilisha mapambazuko mapya kwa Kenya kwani utakuwa na msaada mkubwa sana katika suala la usafiri wa barabara, hasa kwa madereva wanaosafiri kati ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta na wilaya kuu ya biashara ya Nairobi.

Macharia amesema barabara kuu ya Nairobi ni vitega uchumi vya kibinafsi na kwa hivyo serikali haijatoa pesa zozote kwa ujenzi wa huo.

"Serikali ya Kenya haijatoa pesa zozote katika uwekezaji huu, hatujakopa hata senti moja ya jumla ya dola za Kimarekani milioni 600, ambazo ni takriban shilingi bilioni 70," amesema.

Katika kipindi cha ujenzi, barabara hiyo kuu imeleta nafasi za ajira zaidi ya 6,000 za moja kwa moja, na kuwanufaisha wakandarasi wadogo 200 na mamia ya wauzaji wengine wa ndani wa vifaa vya ujenzi kama vile chuma, mchanga na saruji.

Kazi mpya sasa imeibuka nchini Kenya nayo ni ya uhudumu wa kutoza ushuru kwenye barabara hiyo kuu.

Zaidi ya wahudumu 400 wa kutoza ushuru sasa wanafanya kazi katika Barabara Kuu ya Nairobi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha