

Lugha Nyingine
Mji wa Shanghai nchini China warejea katika hali ya kawaida huku maambukizi ya virusi vya Korona yakipungua
![]() |
Watu wakitembelea bustani katika eneo la Xujiahui huko Shanghai, China, Juni 1, 2022. (Xinhua/Liu Ying) |
SHANGHAI - Wakati saa ya Jengo la Forodha la Shanghai nchini China lililoko eneo la Bund ikigonga usiku wa manane, barabara zinazounganisha pande mbili za Mto Huangpu zilikuwa zimefunguliwa kikamilifu, vizuizi katika sehemu kadhaa za mandhari vimeondolewa na magari ya kibinafsi yameanza kuonekana tena kwenye barabara kuu.
Hadi kufikia Jumatano, Juni 1, Shanghai ilikuwa imerejea kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji na maisha ya kawaida baada ya miezi miwili ya usimamizi uliofungwa ili kudhibiti kuibuka tena kwa UVIKO-19.
Serikali ya Mji wa Shanghai jana Jumatano asubuhi ilituma barua mtandaoni ikiwashukuru wakazi wake milioni 25 kwa uungaji mkono na juhudi zao. Barua hiyo ilieleza kwamba baada ya zaidi ya miezi miwili ya mapambano mfululizo dhidi ya UVIKO-19, vita vikali vya kuulinda mji huo vimepata matokeo makubwa, na Shanghai imeingia katika hatua ya kurejesha uzalishaji na maisha ya kawaida.
Zaidi ya visa 600,000 vimeripotiwa katika wimbi hili la hivi majuzi la UVIKO-19. Wagonjwa wengi sasa wameruhusiwa kutoka hospitalini, na Jumanne wiki hii, hospitali kubwa zaidi ya muda ya wagonjwa wa UVIKO-19 huko Shanghai ilifungwa.
"Katika Siku hii maalum ya Watoto, ninaona matumaini zaidi na ninaamini kwamba mimi, familia yangu na mji (wa Shanghai) tunaweza kupata nafuu hatua kwa hatua," amesema Xiao Jing, ambaye yeye na mama yake waliruhusiwa kutoka hospitalini jana Jumatano.
Siku hiyo hiyo, teksi nyingi na huduma za usafirishaji huko Shanghai zilianza tena shughuli za kawaida. Njia zote 20 za treni za chini ya ardhi katika mji huo zilianza tena shughuli kwa sehemu, na vituo vitatu vya reli vilianza tena huduma zao kati ya mikoa.
Hadi kufikia saa sita mchana siku ya Jumatano, maeneo ya katikati mwa Mji wa Shanghai yalishuhudia idadi kubwa ya watu wakizunguka huku na kule, huku majengo yenye maduka makubwa, maduka ya bidhaa na mikahawa ikifunguliwa.
Serikali ya mji huo imesema hivi majuzi kwamba itafanya kila iwezalo kusaidia wafanyabiashara kushinda changamoto zao, kuanza tena uzalishaji na shughuli haraka iwezekanavyo, na kurudisha uchumi na jamii kwenye mstari haraka iwezekanavyo.
Idara ya Afya ya Shanghai imesema, Jumanne wiki hii mji huo uliripoti visa vitano vilivyothibitishwa vya UVIKO-19 na visa 10 vya wagonjwa wasio na dalili.
Hadi Jumanne, idadi ya visa vipya vilivyothibitishwa vya UVIKO-19 huko Shanghai imepungua hadi chini ya kumi kwa siku tatu mfululizo. Wakazi wameonyesha imani katika juhudi za kuzuia na kudhibiti janga hili, na kurejea tena kwa shughuli za uzalishaji.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma