EU yachukua hatua za kisheria dhidi ya Uingereza juu ya mabadiliko kwenye makubaliano ya baada ya Brexit

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 16, 2022
EU yachukua hatua za kisheria dhidi ya Uingereza juu ya mabadiliko kwenye makubaliano ya baada ya Brexit
Magari yakipita kwenye makao makuu ya Kamisheni ya Ulaya huko Brussels, Ubelgiji, Oktoba 8, 2021. (Xinhua/Zheng Huansong)

BRUSSELS - Umoja wa Ulaya (EU) umeanzisha hatua za kisheria dhidi ya Uingereza kufuatia nchi hiyo kuchukua hatua za "upande mmoja" kuandika upya sehemu za itifaki ya Ireland Kaskazini inayohusu makubaliano ya baada ya Brexit, Kamisheni ya Ulaya imesema Jumatano wiki hii.

Kamati ya Utendaji ya EU imesema katika taarifa yake kwamba imefungua kesi za ukiukaji dhidi ya Uingereza "kwa kutofuata sehemu muhimu za Itifaki ya Ireland/Ireland ya Kaskazini" na kwa kushindwa kutekeleza itifaki hiyo licha ya wito wa mara kwa mara.

"Huu ni uvunjaji wa wazi wa sheria za kimataifa," imesema.

Mapema wiki hii, Serikali ya Uingereza ilisema kwamba mswada uliowasilishwa bungneni Juni 13 utairuhusu "kushughulikia shida za kivitendo ambazo itifaki hiyo imesababisha huko Ireland Kaskazini katika maeneo manne muhimu: michakato ya mizigo ya forodha, udhibiti usionyumbulika, tofauti za ushuru na matumizi, na masuala ya utawala wa kidemokrasia."

Hata hivyo, Kamisheni ya Ulaya inaamini kwamba Uingereza inakiuka mikataba ya kimataifa.

"Uaminifu unajengwa kwa kuzingatia wajibu wa kimataifa," Makamu wa Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Maros Sefcovic amesema. "Kuchukua hatua za upande mmoja hakujengi. Kukiuka mikataba ya kimataifa hakukubaliki. Uingereza haiheshimu itifaki."

"Bado ninaamini katika dhamira ya dhati ya kisiasa kufanya itifaki fanye kazi, tunaweza kufikia malengo yetu," ameongeza.

Jumatano wiki hii ilishuhudia kesi mbili mpya za ukiukaji zikifunguliwa dhidi ya Uingereza kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake chini ya sheria za EU za usafi na usalama wa bidhaa (SPS) na kwa kushindwa kuipatia EU data fulani za takwimu za biashara kuhusiana na Ireland Kaskazini, kama inavyotakiwa chini ya itifaki.

Umoja huo wa Ulaya wenye nchi wanachama 27 pia ulianza tena kesi ya ukiukaji iliyofunguliwa dhidi ya Serikali ya Uingereza mwaka jana baada ya kuongezwa kwa muda wa msamaha ambao unatumika kwa biashara katika kisiwa cha Ireland. Kesi hiyo ilisitishwa Septemba 2021 huku pande hizo mbili zikijaribu kutafuta suluhu ya pamoja.

Kesi za ukiukaji zinaweza kuishia kwenye Mahakama ya Haki ya EU.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha