Kongamano la Aswan lafunguliwa nchini Misri likilenga migogoro mbalimbali barani Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 22, 2022
Kongamano la Aswan lafunguliwa nchini Misri likilenga migogoro mbalimbali barani Afrika
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Sameh Shoukry akihutubia mkutano wa tatu wa Kongamano la Amani na Maendeleo Endelevu la Aswan mjini Cairo, Misri, Tarehe 21 Juni 2022. Mkutano wa tatu wa Kongamano la Amani na Maendeleo Endelevu la Aswan limeanza Jumanne wiki hii likilenga mizozo mingi inayokabili Afrika, hasa usalama wa chakula, mabadiliko ya tabianchi na mapambano dhidi ya ugaidi. (Xinhua/Ahmed Gomaa)

CAIRO – Mkutano wa tatu wa Kongamano la Amani na Maendeleo Endelevu la Aswan umefunguliwa Jumanne wiki hii ukilenga misukosuko mingi inayoikabili Afrika, hususan usalama wa chakula, mabadiliko ya tabianchi na mapambano dhidi ya ugaidi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres, amesema katika hotuba yake kwa njia ya video kwenye kongamano hilo linalofanyika Cairo, Mji Mkuu wa Misri kwamba "watu wa Afrika wanakabiliwa na misukosuko ya aina mbalimbali isiyo na kifani".

Guterres amesema, misukosuko hiyo, ni pamoja na mgogoro wa kiuchumi uliosababishwa na janga la UVIKO-19 na kuongezeka kwa bei za bidhaa kulikosababishwa na vita kati ya Russia na Ukraine, suala la upatikanaji usio sawa wa chanjo, mgogoro wa kifedha huku nchi zikikosa kupata msamaha wa madeni, misukosuko ya kukosekana kwa utulivu, ugaidi na vita pamoja na athari za tabianchi.

Guterres ameongeza kuwa bara hilo linahitaji kupanua wigo wa upatikanaji wa fedha na msamaha wa madeni ili liweze kuwekeza katika kutengeneza nafasi za ajira, kupunguza umaskini, ulinzi wa kijamii, usalama wa chakula na ukuaji wa uchumi wa kijani, wakati ambapo vita vya Ukraine pamoja na mabadiliko ya tabianchi na janga la UVIKO-19 vikiliathiri sana.

Katika hotuba yake, Rais wa Misri, Abdel-Fattah al-Sisi, amezungumzia janga la chakula linalokabili Afrika na madhara makubwa ambayo linaweza kusababisha kwenye usalama na utulivu wa jamii za Afrika, na kuzitaka nchi za Afrika zichukue hatua za dharura na madhubuti kwa uratibu wa pamoja na washirika wa kimataifa na jumuiya ya kimataifa.

"Changamoto zinazohusiana na uhaba wa maji na kupanda kwa bei zinatuhitaji kutafuta suluhu za haraka ili kuondokana na janga hili la kimataifa," Sisi ameeleza.

Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) amesema kwenye mkutano huo kuwa AU imeandaa mkakati wa kuongeza maeneo ya kijani na kupunguza utoaji wa hewa ya kaboni, sambamba na kuzisaidia nchi maskini katika kuongeza uwekezaji ili kufikia maendeleo endelevu.

Kongamano hilo la siku mbili linafanyika katika muundo wa mseto chini ya kaulimbiu "Afrika Katika Kipindi cha Hatari Zinazoongezeka na Athari za Tabianchi: Mwelekeo wa Bara lenye Amani, Ustahimilivu na Endelevu."

Gazeti la Serikali ya Misri, Ahran limeripoti kuwa, kongamano hilo linalohudhuriwa na washiriki 900 kutoka nchi 50, linashughulikia vipaumbele kadhaa vya Afrika, vikiwemo kuimarisha ushirikiano katika kupambana na ugaidi, kukabiliana na athari za janga la UVIKO-19, kufikia usalama wa chakula, na kuendeleza juhudi za ujenzi na maendeleo baada ya janga. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha