Mgomo mkubwa zaidi katika miaka 30 wa wafanyakazi wa reli nchini Uingereza wasababisha usumbufu mkubwa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 23, 2022
Mgomo mkubwa zaidi katika miaka 30 wa wafanyakazi wa reli nchini Uingereza wasababisha usumbufu mkubwa
Picha iliyopigwa Tarehe 21 Juni 2022 ikionyesha notisi ya mgomo kwenye Stesheni ya Makutano ya Clapham mjini London, Uingereza. (Picha na Tim Ireland/Xinhua)

LONDON - Baada ya mazungumzo ya mwisho kati ya vyama vya wafanyakazi na waendeshaji reli kuvunjika siku ya Jumatatu, Muungano wa Kitaifa wa Wafanyakazi wa Vyombo vya usafiri wa Reli, Majini na Uchukuzi wa Uingereza (RMT) siku ya Jumanne wiki hii uliidhinisha mgomo mkubwa zaidi wa wafanyakazi wa reli ambao haujawahi kuonekana katika miaka 30 iliyopita ambao unatarajiwa kusababisha usumbufu mkubwa wa huduma za reli nchini Uingereza, Scotland na Wales.

Ni takriban asilimia 20 tu ya treni za abiria ndizo zilipangwa kusafiri baada ya wafanyakazi kuondoka kazini saa 6 siku Jumanne. Mgomo huo utaendelea Alhamisi na Jumamosi wiki hii na kuathiri mamilioni ya abiria.

Zaidi ya wanachama 40,000 wa chama cha RMT, ikiwa ni pamoja na walinzi, wafanyakazi wa upishi, watoa ishara na wafanyakazi wa matengenezo wanashiriki katika mgomo huo.

RMT iko kwenye mgogoro na waendeshaji wa reli kuhusu malipo, pensheni na kupunguzwa kwa wafanyakazi. Watu kote nchini Uingereza wanatatizika na kupanda kwa gharama za maisha na kuona mishahara yao ikimalizwa na mfumuko wa bei. Mwezi Aprili, mfumuko wa bei wa Uingereza ulipanda hadi asilimia 9, na Benki ya Uingereza ilikadiria utafikia kiwango kinachozidi asilimia 10 mwishoni mwa mwaka huu.

Wakati huo huo, kampuni za reli za Uingereza ziko tayari kupunguza wafanyakazi, malipo na pensheni kwani idadi ya abiria wa reli haijarudi katika kiwango cha kabla ya janga la UVIKO-19.

Andrew Haines, Mtendaji Mkuu wa shirika la uendeshaji wa usafiri wa treni nchini Uingereza la Network Rail amesema "anahisi huruma" kwa abiria kutokana na usumbufu huo lakini akailaumu RMT kwa kutokuwa tayari kuafikiana.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amewataka "wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi kukaa chini na Shirika la Network Rail na makampuni ya treni" ili kujadili makubaliano.

Mgomo tofauti pia ulifanyika kwenye treni za ardhini za London Jumanne. Kuna tahadhari kwamba hii inaweza kuwa mwanzo tu wa migomo ya msimu kiangazi, huku walimu na wauguzi pia wakitishia kuchukua hatua za kugoma kutokana na malalamiko kama hayo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha