Wanaanga wa China wa Chombo cha Shenzhou No.13 wakutana na waandishi wa habari baada ya kumaliza karantini na kupumzika vizuri

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 29, 2022
Wanaanga wa China wa Chombo cha Shenzhou No.13 wakutana na waandishi wa habari baada ya kumaliza karantini na kupumzika vizuri
Mkuu wa Kikundi cha Wanaanga wa China, Jing Haipeng (wa kwanza kushoto), akielezea mipango ya kupata unafuu na kufuatilia hali ya afya za wanaanga wa chombo cha Shenzhou No.13 kwenye mkutano na waandishi wa habari hapa Beijing, China Juni 28, 2022. (Xinhua/Guo Zhongzheng)

BEIJING - Wanaanga watatu wa China waliofanya safari kwenye anga ya juu kwa kutumia chombo cha Shenzhou No.13 wamekutana na waandishi wa habari na watu jana Jumanne, ikiwa ni mara ya kwanza kuonekana baada ya kurejea duniani Mwezi Aprili mwaka huu.

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Beijing, Jing Haipeng, Mkuu wa Kikundi cha Wanaanga wa China, alielezea mipango ya kupata unafuu na kufuatilia hali ya afya za wanaanga hao wa Shenzhou No.13.

Jing alisema, wanaanga hao wamekamilisha hatua za kuwekwa karantini na kupumzika vizuri na kuhamia hatua ya uangalizi. Kwa sasa, wako katika hali nzuri ya kimwili na kiakili wakiwa na majibu vipimo yasiyoonesha tatizo lolote la kiafya.

Wanaanga hao kimsingi wamerejea katika hali ya kawaida ya mioyo yao kufanya kazi, amesema Jing, akiongeza kuwa nguvu zao za misuli, ustahimilivu na msongamano wa mifupa vimepona vizuri.

Jing amesema wanaanga hao watatu wataanza tena mafunzo yao ya kawaida baada ya kukamilisha tathmini ya afya.

Kikiwa kilirushwa Oktoba 16, 2021, chombo cha anga ya juu cha Shenzhou No.13 kiliwatuma Zhai Zhigang, Wang Yaping na Ye Guangfu kwenye moduli ya msingi ya kituo cha anga ya juu cha China cha Tianhe, ambako waliishi kwa miezi sita, na kuweka rekodi mpya ya wanaanga wa China kukaa kwa muda mrefu kwenye anga ya juu. Watatu hao walirejea duniani wakiwa salama Aprili 16, 2022.

Wanaanga hao wamekamilisha mfululizo wa majaribio ya kisayansi ya kibunifu na ya msingi na utumizi wa anga ya juu katika hali ya ustawi wanayoelezea kama "kujisikia vizuri."

Zhai Zhigang anakuwa mwanaanga wa kwanza wa China kufanya matembezi kwenye anga ya juu na amefanya shughuli nyingi za ziada kuliko mwanaanga mwingine yeyote wa China. Amesema kuwa hali ya "kujisikia vizuri," katika anga ya juu na wakati wa mafunzo, inafaidika kutokana na maendeleo ya juhudi za nchi ya China katika kuboresha utaalamu wa anga ya juu.

Wang Yaping ndiye mwanaanga wa kwanza wa kike wa China kufanya matembezi ya ziada kwenye anga ya juu na "mwalimu wa kwenye anga ya juu" wa kwanza nchini China, akiwasilisha habari kuhusu mada zinazohusiana na anga ya juu kwa vijana. Matarajio yake ni kuona vijana wakishiriki katika ujenzi wa kituo cha anga ya juu cha China.

Misheni ya Shenzhou-13 ni misheni ya kwanza ya anga ya juu kwa mwanaanga Ye Guangfu. Amesema kituo cha anga ya juu cha China kinakaribisha wanaanga wa kigeni.

Wanaanga hao watatu wamesema wako tayari kurejea angani tena.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha