Makala: Wakulima wa Tanzania wayapenda maziwa ya soya ya China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 05, 2022
Makala: Wakulima wa Tanzania wayapenda maziwa ya soya ya China
Mwanakijiji akinywa maziwa ya soya mjini Morogoro, Tanzania, Juni 23, 2022. Maziwa ya soya ambayo ni kinywaji cha kijadi cha China chenye ladha na lishe, yanazidi kuwa maarufu miongoni mwa Watanzania katika vijiji vya mkoa wa Morogoro, Magharibi mwa Dar es Salaam. (Chuo Kikuu cha Kilimo cha China/Kutumwa kupitia Xinhua)

DAR ES SALAAM – Maziwa ya soya, kinywaji cha kijadi cha China chenye ladha na lishe, yanazidi kuwa maarufu miongoni mwa Watanzania katika vijiji vya Mkoa wa Morogoro, Magharibi mwa Mji Mkuu wa kibiashara wa nchi hiyo, Dar es Salaam.

Pamoja na kwamba maziwa ya soya ni mapya kwa watanzania, wanahisi yana ladha. Tatu Seif, mkulima wa Kijiji cha Kitete mwenye umri wa miaka 62, anasema maziwa ya soya yana ladha nzuri. "Ninayapenda na natumai marafiki zangu watapenda. Ni mazuri kwa afya zetu."

Kuongezeka kwa umaarufu wa kinywaji hiki kipya chenye kusaidia afya kumetokana na mradi wa ubia wa nchi mbili nchini Tanzania, unaoongozwa na mwanasayansi wa kilimo kutoka China Li Xiaoyuan.

Li na timu yake ya wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha China (CAU) waliamua kushirikiana na viongozi wa Mkoa wa Morogoro kuhamasisha mradi wa upandaji kwa pamoja mahindi na soya uitwao "Maharagwe Madogo na Lishe Kubwa". Walichagua vijiji vinne vya mfano vya Peapea, Kitete, Makuyu na Mtegowasimba kama mradi wa majaribio katika mkoa huo.

Chini ya mradi huo, wataalamu hao kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Morogoro walisambaza mbegu za soya kwa wakulima wa vijiji hivyo vinne Januari mwaka huu na kutoa mwongozo wa upandaji na usimamizi mahali hapo.

Hadi mwishoni mwa Mei, msimu wa mavuno wa soya ulianza, na kuwaacha wakulima na tabasamu pana.

Nasoro Athumani mwenye umri wa miaka 60 alitajwa kuwa mkulima bora wa soya katika Kijiji cha Peapea kwa Mwaka 2022 baada ya familia yake kupanda soya kwenye shamba la ekari 0.75, na kuvuna takriban kilo 400 za maharagwe hayo.

“Mwaka ujao ninapanga kupanda soya kwenye ekari mbili,” anasema mkulima huyo huku akiwa na matarajio makubwa.

Li anasema kuwa mahindi ni chakula kikuu barani Afrika wakati soya inaweza kufidia kuongezeka kwa lishe, na ameongeza kuwa kupanda soya katikati ya mahindi kunaweza kuboresha muundo wa lishe wa kijadi kwa ufanisi zaidi.

Naye Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia Sekta ya Uchumi na Uzalishaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Rozalia Grayson Rwegasira, ameipongeza CAU kwa kutambulisha maziwa ya soya mkoani humo, akisema anatarajia mradi huo wa soya utawanufaisha wananchi wengi zaidi hasa watoto na wanawake.

“Maziwa ya soya ni mazuri hasa kwa watoto chini ya miaka mitano, mama wajawazito na wanaonyonyesha ili kuboresha afya zao, mradi huo unatakiwa kuwafikia watu wengi iwezekanavyo,” anasema.

Hii si mara ya kwanza kwa Li Xiaoyun na timu yake kuendesha miradi ya misaada ya kilimo nchini Tanzania.

Tangu Mwaka 2011, CAU imeshirikiana na Serikali ya Mkoa wa Morogoro kutekeleza mradi wa "Mavuno Mengi kwa Teknolojia Ndogo" uliolenga kuongeza uzalishaji wa mahindi na kipato.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha