

Lugha Nyingine
Uwanja wa ndege wa kwanza maalumu kwa ndege za mizigo barani Asia waanza kufanya kazi nchini China
WUHAN - Ndege ya mizigo aina ya Boeing 767-300 ilipaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Ezhou Huahu katika Mkoa wa Hubei, katikati mwa China saa 5:36 asubuhi Jumapili, kuashiria kuanza rasmi kwa shughuli za uwanja wa ndege wa kwanza maalumu kwa ndege za mizigo wa China.
Ukiwa katika Mji wa Ezhou, pia ni uwanja wa ndege wa kwanza maalumu kwa ndege za mizigo barani Asia na wa nne wa aina yake duniani.
Uwanja huo mpya wa ndege, wenye kituo cha mizigo chenye ukubwa wa mita za mraba 23,000, kituo cha kusafirisha mizigo chenye takriban mita za mraba 700,000, stendi 124 za maegesho na njia mbili za kurukia ndege, unatarajiwa kuboresha ufanisi wa usafiri wa mizigo kwa njia ya anga na kuhimiza zaidi ufunguaji mlango nchini China.
“Uendeshaji wa uwanja wa ndege wa Ezhou Huahu unaendana na mahitaji ya maendeleo ya China,” amesema Su Xiaoyan, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Mipango na Maendeleo ya uwanja huo.
Kwa mujibu wa Shirika la Posta la China, idadi ya vifurushi vinavyoshughulikiwa na kampuni za usafirishaji za China ilifikia rekodi ya juu ya zaidi ya bilioni 108 mwaka jana, na inatarajiwa kudumisha ukuaji thabiti mnamo Mwaka 2022.
Kazi za uwanja wa ndege wa Ezhou zimewekwa kwa kulingana na kiwango cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Memphis nchini Marekani, ni moja ya viwanja vya ndege za mizigo vyenye shughuli nyingi zaidi duniani.
Kampuni ya usafirishaji ya SF Express, ambayo ni mtoa huduma mkuu wa China wa ugavi, ina jukumu muhimu katika uwanja wa ndege wa Ezhou, kama ilivyo kwa Kampumni ya FedEx Express inavyoshughulikia mizigo mingi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Memphis.
Mji wa Ezhou usio na bandari uko umbali wa mamia ya kilomita kutoka bandari yoyote. Lakini kutokana na kuanza kazi kwa uwanja huo mpya wa ndege, sasa bidhaa kutoka Ezhou zinaweza kufika popote nchini China kwa usiku mmoja na kwenda ng'ambo kwa siku mbili.
"Kiwanja cha ndege kitahimiza ufunguaji wa eneo la kati la China na nchi nzima," amesema Yin Junwu, Mkurugenzi wa Kamati ya Usimamizi wa Eneo la Kiuchumi la Uwanja wa Ndege wa Ezhou, akiongeza kuwa mashirika ya ndege na makampuni ya meli kutoka Marekani, Ujerumani, Ufaransa na Russia tayari yamefanya mawasiliano ili kuanzisha ushirikiano na uwanja huo wa ndege.
Mbali na usafari wa ndege za mizigo, uwanja huo wa ndege pia hutoa huduma za ndege za abiria kwa Mashariki mwa Hubei. Njia saba za abiria zinazounganisha Ezhou na vituo tisa, ikiwa ni pamoja na Beijing, Shanghai, Chengdu na Kunming, zimeanza kufanya kazi.
Kuwezeshwa na teknolojia nyingi
Ukiwa ndiyo uwanja wa ndege pekee maalumu kwa ndege za mizigo nchini China na barani Asia, Uwanja wa ndege wa Ezhou Huahu umepata mafanikio katika kuendeshwa kidijitali na kwa teknolojia ya akili bandia. Wajenzi wa mradi huo wametuma maombi ya hataza na hakimiliki za teknolojia mpya zaidi ya 70, kama vile 5G, data kubwa, kompyuta ya wingu na akili bandia, kwa ajili ya kufanya uwanja mpya huo wa ndege kuwa salama, kijani na bora zaidi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma