

Lugha Nyingine
Afrika Kusini yaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela kwa kusaidia jamii
![]() |
Wafanyakazi wa kujitolea wakitayarisha chakula cha hisani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela mjini Cape Town, Afrika Kusini, Tarehe 18 Julai 2022. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua) |
JOHANNESBURG - Serikali na raia wa Afrika Kusini Jumatatu wiki hii walisherehekea Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela kwa kusaidia jamii za wenyeji.
Viongozi wa Serikali walitembelea jumuiya mbalimbali kwa ajili ya kutoa misaada kwa wahitaji kupitia matendo ya hisani na maendeleo ya jamii, kuitikia wito uliotolewa na Mandela baada ya kutangazwa kuanzishwa kwa Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela kwamba kila mtu amuenzi kwa kusaidia jamii yake.
Kwa kutambua mchango wa rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini katika utamaduni wa amani na uhuru, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mwaka 2009 liliitangaza Julai 18 ya kila mwaka ambayo ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mandela, kuwa Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela.
Shughuli za mwaka huu za kuadhimisha siku hiyo zilijumuisha upandaji miti ya matunda na miti asilia, pamoja na kuanzisha bustani za chakula ili kuelimisha jamii juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi na usalama wa chakula na zimefanyika chini ya kaulimbiu ya "Fanya uwezavyo, kwa ulichonacho, mahali ulipo."
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa aliongoza maadhimisho hayo huko Gqeberha, Jimbo la Eastern Cape, akijiunga na Kampeni ya Kusafisha mazingira ya Mito.
Huko Orlando Magharibi mjini Johannesburg, ambako Mandela alikuwa akiishi, Zandi Makhanda mwenye umri wa miaka 31 alitoa chakula kwa wanajamii wenye uhitaji.
"Tumekuwa tukitembelea jamii katika siku chache zilizopita ili kujiandaa kwa siku hii na ninafurahi kutumia siku hii kwa manufaa kwa kuwasaidia wengine," alisema.
Lilian Shandu mwenye umri wa miaka 29, mkazi katika eneo la Centurion la Mji wa Tshwane, alitoa vitabu kwa watoto wadogo. Kundi la marafiki wapenda vitabu walikuja na wazo la kukusanya vitabu kwa ajili ya watoto ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwanunulia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma