Ulaya yaingia kipindi cha joto kali katika historia likisababisha kulipuka kwa moto sehemu nyingi, na kuua mamia ya watu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 20, 2022
Ulaya yaingia kipindi cha joto kali katika historia likisababisha kulipuka kwa moto sehemu nyingi, na kuua mamia ya watu
Watalii wakipoza miili yao kwenye chemchemi ya maji iliyopo Piazza di Spagna huko Roma, Italia Julai 17, 2022. (Picha na Alberto Lingria/Xinhua)

BRUSSELS - Mawimbi ya joto yanayokumba maeneo ya Magharibi na Kusini mwa Ulaya hayaonyeshi dalili ya kupungua. Rekodi za halijoto zinatarajiwa kuonyesha kuongezeka tena katika baadhi ya nchi na jua kali limesababisha mamia ya watu kupoteza maisha na kuchochea moto mkali wa nyika.

Idara ya hali ya hewa la Uingereza (Met Office) imeonya kwamba nchi hiyo inaweza kushuhudia siku yake ya joto zaidi katika rekodi wiki hii huku halijoto ikitarajiwa kufikia rekodi ya nyuzi joto 40 katika maeneo mengine.

Idara hiyo imetoa tahadhari yake ya kwanza nyekundu kuhusu joto kali, na kuukumbusha umma kwamba joto hilo linaleta hatari ya ugonjwa mbaya au hata hatari ya kupoteza maisha.

Rekodi ya sasa ya joto la juu nchini Uingereza ni nyuzi joto 38.7 iliyorekodiwa Julai 2019.

Kituo cha habari za kila siku cha Ufaransa cha BFMTV kiliripoti Jumatatu wiki hii kwamba idara za hali ya hewa za Magharibi mwa Ufaransa zinaendelea kutoa tahadhari ya "joto kali", huku halijoto ikitarajiwa kufikia nyuzi joto 40.

Wizara ya afya ya Hispania ilisema Jumatatu wiki hii kuwa watu 510 walipoteza maisha kutokana na sababu zinazohusiana na joto katika wiki ya kwanza ya wimbi la joto wakati zebaki ilipofikia digrii 45 Selcius katika baadhi ya maeneo ya nchi.

Joto hilo linawaathiri hasa wazee, ambapo waathiriwa 321 kati ya 510 ni wenye umri wa miaka 85 au zaidi, 121 ni wenye umri wa miaka 75-84, na 44 ni wenye umri wa miaka 65-74.

Ripoti ya hivi karibuni ilitolewa na Kituo cha Pamoja cha Utafiti cha Kamisheni ya Ulaya ilionyesha kuwa karibu nusu ya eneo la Umoja wa Ulaya (EU) na Uingereza ziko katika hatari ya ukame mwezi Julai. Hali ya ukame na uhaba wa maji vinaathiri uzalishaji wa nishati na kupunguza mavuno ya mazao.

Joto na ukame huo pia husababisha moto mkali katika nchi mbalimbali zikiwemo Ufaransa, Hispania, Ureno, Italia na Ugiriki.

BFMTV imeripoti kwamba moto wa nyika unaoendelea Kusini Magharibi mwa Ufaransa tangu Julai 12 umeharibu hekta 14,000 za ardhi na watu 16,200 wamelazimika kuyahama makazi yao. Takriban askari wa zima moto 1,700 bado wanajaribu kuzima moto huo lakini wimbi la joto na upepo mkali unafanya kazi yao kuwa ngumu.

Idara ya Dharura ya Hispania imesema, moto wa nyika nchini humo umeteketeza zaidi ya hekta 22,000 za misitu na vichaka wakati wa wimbi la joto.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, ili kupunguza hatari ya kuongezeka kwa moto mkali, EU iko kwenye mipango ya kununua ndege za kuzima moto.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha