Mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa wahamasisha uungwaji mkono kwa maendeleo endelevu ya Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 22, 2022
Mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa wahamasisha uungwaji mkono kwa maendeleo endelevu ya Afrika
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed (kati, kwenye skrini) akitoa risala kwenye mazungumzo maalum ya ngazi ya juu yenye mada ya "Afrika Tunayoitaka: Kuthibitisha Upya Maendeleo ya Afrika kuwa Kipaumbele cha Mfumo wa Umoja wa Mataifa" kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Julai 20, 2022. Afrika iliangaziwa kwenye mazungumzo maalum wa ngazi ya juu yaliyofanyika Jumatano wiki hii kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, ambayo yalikuwa na lengo la kuhamasisha uungwaji mkono zaidi kwa Afrika kwa ajili ya kuhimiza maendeleo endelevu ya bara hilo. (Mark Garten/Picha ya UN/Kutumwa kupitia Xinhua)

UMOJA WA MATAIFA - Afrika iliangaziwa kwenye mazungumzo maalum ya ngazi ya juu yaliyofanyika Jumatano wiki hii kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, ambayo yalilenga kuhamasisha uungwaji mkono zaidi kwa ajili ya kuhimiza maendeleo endelevu ya Afrika.

Mkutano huo wa siku moja iliitishwa kwa pamoja na marais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC) ukiwa na kaulimbiu ya "Afrika Tunayoitaka: Kuthibitisha Upya Maendeleo ya Afrika yakiwa Kipaumbele cha Mfumo wa Umoja wa Mataifa."

"Leo hii, tunaangazia Afrika, bara ambalo lina utajiri mkubwa wa rasilimali ya watu na ya asili na uwezo mkubwa wa kiuchumi na kijamii ambao haujatumika, lakini bado linakabiliwa na changamoto katika kutimiza malengo ya maendeleo," amesema Abdulla Shahid, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Akielezea maendeleo endelevu ya Afrika kama "kipaumbele" kwa Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa”, Abdulla amesisitiza kuwa hatua za pamoja mara nyingi zimekuwa pungufu katika kufikia mafanikio.

Katika hotuba yake, Rais wa ECOSOC Collen Vixen Kelapile amesema mazungumzo hayo ya ngazi ya juu "yamefanyika kwa wakati muafaka na ni muhimu", huku akibainisha kuwa yameitishwa ili kuweka maendeleo endelevu ya Afrika katika kiini cha kazi ya Umoja wa Mataifa.

Akihutubia kwenye mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed amesema mazungumzo hayo ya ngazi ya juu yanatoa jukwaa la kimataifa kwa nchi wanachama wa Afrika na Umoja wa Mataifa na washirika wenzi kushirikishana maendeleo na kuthibitisha kwamba kutoa mwanga kwa dira ya maendeleo ya Afrika "kunabakia kuwa kipaumbele chetu cha pamoja."

Mohammed, ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ameeleza kwamba mafanikio ya maendeleo ya Afrika yako hatarini, kutokana na athari za migogoro mitatu inayoendelea sasa -- janga la UVIKO-19, mabadiliko ya tabianchi na mgogoro kati ya Russia na Ukraine.

Hata hivyo, "Afrika tunayoitaka bado inaweza kufikiwa," amesema. "Ili kufika huko, tunahitaji kubadilisha mitazamo yetu na kugeuza migogoro hiyo mitatu kuwa fursa."

Kwa ajili hiyo, Mohammed amesisitiza masuala matano muhimu, ikiwa ni pamoja na kujenga mifumo ya sera na taasisi zenye ufanisi na zinazotegemeka, kuwekeza katika mawasiliano na teknolojia ya kidijitali, kuboresha elimu na maendeleo ya ustadi, kufikia nishati endelevu kwa wote katika bara zima, pamoja na mtazamo wa jumla wa kutafuta mitaji.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha