China yarusha moduli ya kwanza ya maabara kwenye kituo cha anga ya juu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 25, 2022
China yarusha moduli ya kwanza ya maabara kwenye kituo cha anga ya juu
Roketi ya Changzheng-5B Y3, iliyobeba chombo cha maabara ya Wentian, ikirushwa kutoka kwenye Eneo la Urushaji wa Vyombo kwenye Anga ya Juu la Wenchan, Mkoa wa Hainan, Kusini mwa China, Julai 24, 2022. (Xinhua/Li Gang)

WENCHANG, Hainan - China Jumapili imerusha Wentian, moduli ya kwanza ya maabara ya kituo chake cha anga ya juu. Moduli hiyo mpya itafanya kazi kama nakala rudufu ya moduli ya msingi na kama jukwaa lenye nguvu la majaribio ya kisayansi.

Bw.Liu Gang, Naibu Mbunifu Mkuu wa mfumo wa kituo cha anga za juu cha China anayetokea Taasisi Kuu ya Sayansi ya Anga ya Juu ya China alisema, moduli hiyo ya Wentian ina urefu wa mita 17.9, kipenyo cha juu cha mita 4.2, na uzito wa tani 23 za kupaa.

Idara ya Anga za Juu ya China imesema katika taarifa yake kuwa, roketi ya Changzheng-5B Y3, iliyobeba moduli ya Wentian, ilirushwa kutoka Eneo la Urushaji wa Vyombo kwenye Anga ya Juu la Wenchan, lililoko kwenye pwani ya Mkoa wa Kisiwa cha Hainan.

Ujenzi wa kituo cha anga za juu cha China cha Tiangong unatarajiwa kukamilika mwaka huu. Kisha kitabadilika kutoka kwa muundo wa moduli moja hadi maabara ya anga ya taifa yenye moduli tatu -- moduli ya msingi, Tianhe, na moduli mbili za maabara, Wentian na Mengtian.

Moduli ya Tianhe ilirushwa Aprili 2021, na moduli ya Mengtian imepangwa kurushwa kwenye anaga ya juu Mwezi Oktoba mwaka huu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha