IMF yapunguza makadirio ya kukua kwa uchumi duniani Mwaka 2022 hadi asilimia 3.2

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 27, 2022
IMF yapunguza makadirio ya kukua kwa uchumi duniani Mwaka 2022 hadi asilimia 3.2
Picha iliyopigwa Aprili 19, 2022 ikionyesha Makao Makuu ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) huko Washington, D.C., Marekani. (Picha na Ting Shen/Xinhua)

WASHINGTON - Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Jumanne wiki hii limepunguza makadirio ya kukua kwa uchumi duniani kwa Mwaka 2022 hadi asilimia 3.2, ikiwa ni chini kwa asilimia 0.4 kutoka makadirio ya Mwezi Aprili, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Mtazamo wa Uchumi wa Dunia (WEO).

Ripoti hiyo inaonesha kuwa, mishtuko kadhaa imeathiri uchumi wa Dunia ambao tayari umedhoofishwa kutokana na janga la UVIKO-19, pamoja na mfumuko wa bei wa juu duniani kuliko ilivyotarajiwa - haswa nchini Marekani na nchi za Ulaya zenye uchumi mkubwa - na kusababisha hali ngumu ya kifedha, na athari mbaya zaidi kutoka kwenye mgogoro wa Ukraine.

Uchumi wa Dunia "unakabiliwa na mtazamo unaozidi kuwa mbaya na usio na uhakika," Mchumi Mkuu wa IMF Pierre-Olivier Gourinchas alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari Jumanne, akibainisha kuwa hatari nyingi zilizoangaziwa kwenye WEO ya IMF ya Aprili zimeanza kutimia.

Makadirio ya mfumuko wa bei duniani yamerekebishwa kwenda juu kutokana na bei za vyakula na nishati, na unatarajiwa kufikia asilimia 6.6 katika nchi zilizoendelea na asilimia 9.5 katika nchi zenye masoko yanayoibukia na nchi zinazoendelea mwaka huu – ikiwa ni marekebisho ya kupanda juu kwa asilimia 0.9 na 0.8 mtawalia.

“Kwa siku zijazo, ni wazi kwamba benki kuu kuendelea kutekeleza sera kali za kifedha kutakuwa na athari inayoendelea kwa Dunia nzima,” amebainisha Gourinchas.

Gourinchas amesema, kwanza, kutakuwa na kupungua kwa mahitaji na shughuli za kiuchumi katika ngazi ya kimataifa, pili, sera kali za kifedha za benki kuu za Marekani na za nchi nyingine pia zitasababisha kuongezeka kwa thamani ya dola ya Marekani dhidi ya sarafu za nchi zenye masoko yanayoibukia, na kuongeza shinikizo la mfumuko wa bei katika nchi hizi, Tatu, kuna tabia ya jumla ya wawekezaji kuhama kutoka kwenye nchi zenye masoko yanayoibukia na kutafuta maeneo salama.

Amebainisha kuwa hatari kwa mtazamo "zimeunganishwa na kushuka chini kwa uchumi."

Amesema, hatari mbaya za uchumi kwenda chini ni pamoja na: mgogoro wa Ukraine unaweza kusababisha kusimamishwa ghafla kwa usafirishaji wa gesi kwenda Ulaya kutoka Russia, mfumuko wa bei unaweza kubaki juu ikiwa masoko ya ajira yatabaki kuwa magumu kupita kiasi au matarajio ya kupunguza mfumuko wa bei yanaweza kuthibitisha gharama kubwa zaidi kuliko ilivyotarajiwa.

Mchumi huyo amesema, katika hali mbadala inayowezekana ambapo baadhi ya hatari hizi zitatokea, mfumuko wa bei utapanda na ukuaji wa uchumi wa Dunia utapungua zaidi hadi takriban asilimia 2.6 mwaka huu na asilimia 2 mwaka ujao – mwenendo ambao ukuaji wa uchumi umeshuka chini mara tano tangu Mwaka 1970.

Kwa mujibu wa WEO, biashara ya kimataifa inatarajiwa kukua kwa asilimia 4.1 Mwaka 2022 na asilimia 3.2 Mwaka 2023, ikiwa ni kiwango cha chini kwa asilimia 0.9 na asilimia 1.2 mtawalia kutoka makadirio ya Mwezi Aprili.

"Tutakuwa na mabadiliko katika biashara ya kimataifa na hiyo inaweza kutokea baada ya Mwaka 2023," amesema. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha