Benki Kuu ya Marekani yaongeza kiwango cha riba kwa pointi 75 huku kukiwa na mfumuko wa bei unaoongezeka

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 28, 2022
Benki Kuu ya Marekani yaongeza kiwango cha riba kwa pointi 75 huku kukiwa na mfumuko wa bei unaoongezeka
Mwenyekiti wa Benki Kuu ya Marekani Jerome Powell akihudhuria mkutano na waandishi wa habari mjini Washington, D.C., Marekani, Tarehe 27 Julai 2022. (Xinhua/Liu Jie)

WASHINGTON- Benki Kuu ya Marekani Jumatano wiki hii ilipandisha kiwango chake cha riba kwa pointi 75 za msingi, ikiwa ni mara ya pili mfululizo kupandishwa kwa ukubwa huo, kwani mfumuko wa bei unaoongezeka haukuonyesha dalili za wazi za kulegeza.

"Mfumuko wa bei bado umeendelea kuwa juu, unaonyesha kukosekana kwa usawa kwenye utoaji wa bidhaa na mahitaji kunakohusiana na janga la UVIKO-19, bei ya juu ya chakula na nishati, na shinikizo kubwa la bei," Benki Kuu hiyo ya Marekani imesema katika taarifa yake baada ya mkutano wa kisera wa siku mbili, na kuongeza kuwa benki kuu "iko makini sana na hatari ya mfumuko wa bei."

"Vita (nchini Ukraine) na matukio yanayohusiana yanaleta shinikizo la juu la mfumuko wa bei na inatia uzito kwenye shughuli za kiuchumi duniani," Benki Kuu ya Marekani imesema.

Kamati ya Benki Kuu ya Marekani ya Soko Huria (FOMC), ambacho ni chombo cha kuunda sera cha Benki Kuu ya Marekani, iliamua kuongeza kiwango lengwa kwa fedha za Serikali Kuu kutoka asilimia 2.25 hadi 2.5 na "inatarajia kwamba ongezeko linaloendelea katika viwango lengwa litakuwa linalofaa."

Taarifa hiyo ilionyesha kuwa wajumbe wa kamati wote 12 walipiga kura kuunga mkono uamuzi huo.

Hatua hii mpya inakuja baada ya Benki Kuu ya Marekani kuongeza kiwango cha riba chake kwa pointi za msingi 75 katika mkutano wake wa Juni, kuashiria kuongezeka kwa kiwango kikubwa zaidi tangu Mwaka 1994. Benki hiyo hapo awali iliongeza kiwango cha riba kwa pointi za msingi 25 Mwezi Machi na kisha kwa pointi za msingi 50 Mwezi Mei.

Kiashiria cha bei ya wanunuzi bidhaa (CPI) kimebakia zaidi ya asilimia 8 tangu Machi mwaka huu, ikiwa ni ishara mbaya kwamba Benki Kuu ya Marekani ina safari ndefu ya kuleta mfumuko wa bei chini ya udhibiti.

"Ingawa ongezeko lingine kubwa lisilo la kawaida linaweza kuwa muafaka katika mkutano wetu ujao, huo ni uamuzi ambao utategemea takwimu tunazopata kati ya kipindi cha sasa na baadaye," Mwenyekiti wa Benki Kuu ya Marekani, Jerome Powell amesema Jumatano alasiri kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Powell amepuuzia mbali maoni kwamba uchumi wa Marekani tayari uko katika mdororo, akitoa mfano wa nguvu ya soko la ajira.

"Hatujaribu kuingia kwenye mdororo wa uchumi na hatufikirii kuwa lazima," amesema, huku akikiri kwamba njia ya kuepuka mdororo wa uchumi imepungua na inaweza kuwa nyembamba zaidi. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha