Takriban watu 19 wameuawa na wengine 23 kujeruhiwa katika mashambulizi ya bomu nchini Somalia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 29, 2022
Takriban watu 19 wameuawa na wengine 23 kujeruhiwa katika mashambulizi ya bomu nchini Somalia
Picha hii kutoka maktaba iliyopigwa Novemba 20, 2021, ikionyesha mabaki ya gari baada ya shambulio la bomu la kujitoa mhanga huko Mogadishu, Mji Mkuu wa Somalia. (Picha na Hassan Bashi/Xinhua)

MOGADISHU – Maafisa wa Serikali ya Somalia wamesema, takriban watu 19 wameuawa na wengine 23 kujeruhiwa katika mashambulizi tofauti ya mabomu yaliyotokea Jumatano wiki hii katika miji miwili ya Kusini mwa Somalia.

Katika tukio la kwanza, watu 13 walipoteza maisha huku wengine watano wakijeruhiwa baada ya mshambuliaji wa kujitoa mhanga kujilipua katika Mji wa Marka, Mkoa wa Lower Shabelle.

Afisa mmoja wa mkoa huo pia amethibitisha kuwa watu sita waliuawa huku wengine 18 wakijeruhiwa katika mashambulizi mawili kwenye mji wa Afgoye.

Gavana wa mkoa huo Ibrahim Aden Ali Naja amesema mshambuliaji wa kujitoa mhanga aliyekuwa amevalia fulana yenye vilipuzi alijilipua nje ya ofisi ya utawala katika Mji wa Marka na kuua Mkuu wa Wilaya Abdullahi Ali Wafow na wengine 12.

"Wafow aliuawa katika mlipuko huo pamoja na watu wengine 12 ambao alikuwa akizungumza nao nje ya ofisi yake," Naja amewaambia waandishi wa habari mjini Mogadishu, Somalia.

Kundi la wanamgambo wa al-Shabab ambalo limekuwa likiilenga Serikali ya Somalia katika mashambulizi ya karibu kila siku nchini kote limedai kuhusika na shambulio hilo katika Mji wa Marka.

Katika shambulio la pili, afisa mmoja amesema watu sita wameuawa katika milipuko miwili ya barabarani kwenye soko la ndani katika Mji wa Afgoye katika mkoa huo huo.

Msemaji wa zamani wa Mamlaka ya wilaya ya Afgoye Abdukadir Idle ambaye alikuwa katika eneo la tukio amesema mabomu mawili ya ardhini yaliyoendeshwa kutokea mbali yalilipuka katika soko hilo lililokuwa limejaa watu. Idle amebainisha kuwa mlipuko wa pili ulitokea dakika chache baadaye na kuwalenga watu waliokuwa katika shughuli za uokoaji.

"Takriban watu sita, wengi wao wakiwa raia, wameuawa na wengine 18 kujeruhiwa katika mashambulizi mawili yaliyofanywa kupitia vilipuzi vinavyoendeshwa kutokea mbali katika soko la mifugo la Afgoye, mlipuko wa pili umesababisha hasara zaidi," Idle ameliambia Shirika la Habari la Somalia.

Amesema mara nyingi soko hilo huwa na idadi kubwa ya watu wanaofika kununua mifugo Jumatano, ambayo ni siku ya soko.

Kundi hilo la wanamgambo limeongeza mashambulizi huku vikosi vya serikali vikifanya operesheni kali dhidi ya wanamgambo hao wenye itikadi kali kwenye mikoa ya Kati na Kusini katika miezi ya hivi karibuni katika jaribio la kuwaondoa wanamgambo wa al-Shabab.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha