Makala: Njia ya Hariri, historia ya usaarabu wa Dunia na Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 02, 2022
Makala: Njia ya Hariri, historia ya usaarabu wa Dunia na  Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”
Sanamu ya Zhang Qian aliyekuwa mwanzilishi wa Njia ya Hariri ikiwa kwenye bustani jirani na Jumba la Makumbusho yake huko Changgan, Eneo la Hanzhong, Mkoa wa Shaanxi, China (Picha, People’s Daily Online)

Katika siku za hivi karibuni Njia ya Hariri imekuwa ikitajwa na kuandikwa kwenye vyombo vya habari duniani kote. Aidha, Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” limeifanya “Njia ya Hariri” kuwa maarufu zaidi. Wanazuoni, watafiti na wasomi mbalimbali wametumia muda mwingi kufuatilia na kuchapisha maandishi mbalimbali kuhusu Njia ya Hariri. Je unafahamu historia na msingi wa Njia ya Hariri? Je inahusiana vipi na Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”?

Historia yenye utajiri na ustaarabu wa Dunia

Zhang Qian aliyekuwa mwanadiplomasia nguli kutoka Enzi ya Han ya China ya Kale ndiye muasisi wa njia ya hariri. Akiwa amepewa jina la “gwiji wa diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa”, Zhang Qian alitumwa na Wafalme mbalimbali waliowahi kuongoza Enzi ya Han.

Mathalani, Mwaka 138 KK, Mfalme Wudi wa Enzi ya Han alipanga kutuma mjumbe wa kwenda kutafuta uungaji mkono kutoka himaya zingine za Asia ya Kati wakati huo kukiwa na hali ya vita. Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizoko kwenye Jumba la Kumbukumbu la Zhang Qiang lililoko Changgan, Eneo la Hanzhong, Mkoa wa Shaanxi wa China, Zhang Qian akiwa na matarajio makubwa ya kufanya kazi hiyo aliitikia wito huo kutokea Chenggu (Chenggu, Shaanxi) kuanza safari hiyo ngumu akiwa na wanajeshi 100.

Zhang Qian alikuwa na ustadi mkubwa katika kutembelea maeneo mbalimbali ya Asia ya Kale. Safari hii ilitoa mchango mkubwa katika kuhimiza mabadilishano kati ya Enzi ya Han na maeneo ya Magharibi. Aidha, inaelezwa kuwa safari muhimu katika kuunganisha ustaarabu na utamaduni wa Mashariki na ule wa Magharibi.

Baada ya safari hiyo, Zhang Qian alifanya safari nyingi kutokea Enzi ya Han hadi maeneo mengi ya Ulaya-Asia na Magharibi kwa ujumla.

Maofisa na kumbukumbu zilizopo kwenye Jumba la Makumbusho ya Zhang Qian zinaeleza kwamba, baada ya safari hizo za Zhang Qian, mawasiliano kati ya Nyanda za Kati na Magharibi yalianza kuwa ya mara kwa mara. Na biashara kati ya pande hizo ilishamiri na moja ya bidhaa zilizokuwa maarufu ni Hariri. Hivyo kuanza safari za pande mbalimbali zilitengeneza Njia za Hariri.

Njia ya Hariri na Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”

Wakati akitangaza Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, Rais wa China Xi Jinping alisema kuwa, miaka 2000 iliyopita mababu zetu walisafiri na kupita nyika na majangwa ili kufungua mawasiliano na mabadilishano yanayounganisha Asia, Ulaya na Afrika. Xi alisema, njia hiyo kwa sasa inaitwa Njia ya Hariri.

Alisema kuwa, kwa kupitia safari za maelfu ya maili na miaka, njia za kale za hariri zinajumuisha roho ya amani na ushirikiano, uwazi na shirikishi, kufundishana na kunufaishana. Moyo wa Njia ya Hariri umekuwa urithi mkubwa wa ustaarabu wa binadamu.

“Historia ni mwalimu wetu bora. Utukufu wa njia za kale za hariri unaonyesha kwamba umbali wa kijiografia hushindwa. Ikiwa tutachukua hatua ya kwanza ya kuelekea kwa kila mmoja, tunaweza kuanza njia inayoongoza kwa urafiki, maendeleo ya pamoja, amani, maelewano na maisha bora ya baadaye” Xi alisema.

Hapo ndipo Rais Xi, alitangaza Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”. Likiwa na lengo la kufufuka kwa Njia za Kale za Hariri. Kuiunganisha Dunia kwa ustaarabu wake mbalimbali, kuhimiza maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia. Kujenga jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.

Leo hii pendekezo hilo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” limekuwa ni nguvu na uhai mpya katika kujenga Dunia bora. Kutoka Afrika hadi Ulaya, Asia hadi Ulaya na Bara Amerika, pendekezo hili limeamsha ari kubwa ya matumaini ya baadaye.

Dunia sasa imeunganishwa kuliko ilivyokuwa awali. Tofauti na ilivyokuwa enzi za Zhang Qian ambaye alilazimika kufanya safari ngumu na za kutisha kutokana na ugumu wa njia na teknolojia duni, leo “Ukanda Mmoja, Njia Moja” umeleta mageuzi makubwa kwenye Njia ya Hariri. Miundombinu ya kisasa kuanzia reli ya kutoka Asia hadi Ulaya, Reli ya kutoka Tanzania hadi Zambia, Reli ya Ethiopia-Djibouti, Reli ya Mombasa-Nairobi ya Kenya, miundombinu ya majengo, bandari, barabara, na ile ya majini na angani, imeifanya Dunia kuwa kijiji na kuifanya ndoto ya Zhang Qian kuendelea kuwa hai. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha