Viwanda vitatu muhimu vya malighafi ya chuma vinavyofungua Mkoa wa Shaanxi kuingia Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja

By Aris (Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 04, 2022
Viwanda vitatu muhimu vya malighafi ya chuma vinavyofungua Mkoa wa Shaanxi kuingia Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja
Fundi mwanamke kwenye Kiwanda cha Kampuni ya Qinchuan cha kutengeneza mashine nzito na roboti za viwandani akifuatilia utenda kazi wa mashine kiwandani huko Baoji, Mkoa wa Shaanxi, nchini China (Picha na People’s Daily Online)

Mkoa wa Shaanxi nchini China kihistoria ni mwanzilishi wa Njia ya Hariri, njia ambayo katika miaka ya hivi karibuni imehuishwa, kufufuliwa na kuendelezwa chini ya Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”. Katika rekodi za kihistoria, Mwanadiplomasia nguli kutoka Enzi ya Han ya China ya Kale, Zhang Qian ndiye aliyeanza kufanya safari za kidiplomasia na zenye kuhusisha mabadilishano ya kibiashara na ustaarabu wa utamaduni kutoka Mashariki hadi Magharibi.

Safari hizo zikihusisha mifumo ya kijadi ya usafiri kama vile farasi, zilipita kwenye nyika, majangwa na mazingira mengine magumu, kutoka Enzi ya Han hadi maeneo ya Asia, Ulaya, Mashariki ya Kati, Afrika na maeneo mengine.

Njia hizo ambazo zilitumika kusafirisha bidhaa mbalimbali kama vile vitunguu swaumu, karoti, pilipili na hariri katika enzi hizo, sasa Rais Xi Jinping wa China chini ya Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja amezifanya kuwa mpya na za kisasa zikitumika katika kunufaisha Dunia katika sekta zote kuanzia diplomasia, miundombinu, uchumi, jamii na zaidi katika teknolojia.

Mkoa wa Shaanxi nao umechukua fursa hiyo ya “Ukanda Mmoja, Njia Moja” katika kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi ya chuma. Viwanda hivyo vikiwemo vya kutengeneza mitambo, mashine, roboti za viwandani, magari, mataaluma ya reli na kadhalika vimekuwa ni injini ya kuendesha uchumi wa Dunia kwa kusambaza bidhaa katika nchi na maeneo mbalimbali. Viwanda vitatu muhimu vya Mkoa wa Shaanxi, nchini China katika sekta ya chuma ni kama vifuatavyo:

1. Kiwanda cha Magari cha Baoji Geely

Kiwanda hiki ni bingwa wa kuunda magari ya aina mbalimbali. Mathalani gari aina ya Proton X70 ambalo limeundwa chini ya msingi wa Boyue limekuzwa sana katika nchi ya Malaysia. Gari la Volvo nalo linaloundwa na kiwanda hiki limekuwa ni mfano wa ushirikiano kati ya China an Ulaya na limefufua magari aina ya Volvo ambayo yalikuwa yameanza kupoteza umaarufu.

Kiwanda hiki pia kina miradi mingine kama vile Mkakati wa Lynk & Co’s wa Ulaya na Mpango wa Asia-Pasifiki wa kuhimiza uzalishaji kwa teknolojia za hali ya juu, kushiriki katika kubadili mfumo wa sekta ya magari, mradi wa Taxi wa London, Uingereza unaobadili usafiri wa London. Kampuni hii pia ina mitambo Sudan, Ethiopia na Misri.

Habari kutoka kwenye kiwanda hiki zinasema, kiwanda hiki kilichukua fursa ya “Ukanda Mmoja, Njia Moja” kushiriki kwa kunyumbulika na kimuundo, huku kikitumia umaalumu wake wa bidhaa mbalimbali na uwepo wa soko katika nchi zilizoko kando kando za “Ukanda Mmoja, Njia Moja”.

Katika karakana nne kuu za ufundi na vifaa anuwai kwenye kiwanda hiki magari zaidi ya 100,000 yanaundwa kikamilifu kila mwaka. Ndani ya kipindi cha miaka sita iliyopita, imetoa magari 803,900 na kuzalisha thamani ya pato la jumla ya Yuan bilioni 73.7.

2. Kampuni ya Qinchuan

Kiwanda hiki kimejikita katika kutengeneza zana za mashine na roboti za kurahisisha ufanyaji kazi kwenye viwanda. Kampuni hii inaelezwa kuwa uti wa mgongo wa tasnia ya zana za mashine ya China, utafiti na uanzishaji wa teknolojia mpya (R&D) ya China na msingi wa utengenezaji wa zana za mashine za CNC na zana ngumu.

Habari zilizotolewa na vyombo vya habari vilisema kuwa, tangu ujenzi wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” ulipoanzishwa, Kiwanda cha Qinchuan kimeunganishwa kikamilifu katika mkakati wa China wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja”, kimeboresha ufahamu wa chapa zake na ushindani kwa kuhimiza maeneo mapya ya ukuaji wa biashara.

Kampuni hiyo imesaini makubaliano ya mfumo wa ubia na Russia ili kufanikisha uzalishaji wa ndani wa zana za mashine, imeanzisha kituo cha huduma ya masoko ya ng'ambo nchini Afrika Kusini, imeanzisha mashirika ya mauzo nchini Russia, Vietnam na nchi nyingine, na kuimarisha mauzo ya bidhaa.

Kwa mujibu wa takwimu, tangu Mwaka 2020, mauzo ya nje ya Kampuni ya Qinchuan yalikua na kufikia zaidi ya 70%, haswa katika nchi za Uturuki, India na nchi jirani na Russia, kiasi cha biashara kimeongezeka kwa zaidi ya 100%. Mwaka 2021, kiasi cha uagizaji na usafirishaji kilifikia Yuan milioni 350, na kinatarajiwa kuongezeka kwa zaidi ya 20% mwaka huu.

3. Shirika la Reli la China Tawi la Baoqiao

Hii ni kampuni tanzu ya Shirika la Reli la China, ikitajwa kuwa moja ya makampuni 500 bora zaidi duniani. Aidha, ni kampuni kubwa ya Shirika la Reli la China katika teknolojia ya hali ya juu. Hujihusisha na uzalishaji wa bidhaa zinazohusiana na reli, vifaa vya usafiri wa reli, mashine kubwa za kunyanyua na bidhaa nyinginezo.

Viongozi wa Kampuni hiyo wanaeleza kuwa sambamba na mpango wa China wa ujenzi wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, Kampuni ya Reli ya China Baoqiao inashiriki kikamilifu katika ujenzi wa reli nchini China, usafiri wa majini na mitandao mingine ya usafirishaji na uunganishaji wa nchi na maeneo mbalimbali ili kuhakikisha uhimizaji wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja".

Kampuni hiyo inaeleza kuwa tayari imeshafanya biashara na kushirikiana na nchi nyingi duniani zikiwemo za Afrika kama vile Tanzania, Kenya, Zambia, Sierra Leone, Misri, Angola, Afrika Kusini na nyingine nyingi. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha