Umoja wa Mataifa waonya juu ya hatari ya kutokea njaa nchini Somalia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 07, 2022
Umoja wa Mataifa waonya juu ya hatari ya kutokea njaa nchini Somalia
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura Martin Griffiths akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani Machi 15, 2022. (Eskinder Debebe/Picha/Kutumwa na UN kupitia Xinhua)

MOGADISHU – Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa, Martin Griffiths Jumatatu wiki hii ameonya kuhusu msukosuko wa kibinadamu katika nchi ya Somalia, akisema nchi hiyo iko kwenye hatari ya kuingia kwenye baa la njaa kwa mara ya pili tangu Mwaka 2011.

Griffiths amesema kwenye mkutano wa waandishi wa habari mjini Mogadishu, mji mkuu wa Somalia kwamba ukame mkubwa unaoikumba nchi hiyo huenda ukasababisha baadhi ya maeneo ya nchi hiyo kukumbwa na njaa ifikapo mwisho wa Mwaka 2022.

"Njaa iko mlangoni, na leo tunapokea tahadhari ya mwisho. Nimeshtushwa sana siku hizi chache zilizopita na kiwango cha uchungu na mateso tunayoona Wasomali wengi wakikakabiliana nayo," Griffiths amesema mwishoni mwa ziara yake ya siku tano nchini Somalia.

Ripoti ya Uchambuzi wa Usalama wa Chakula na Lishe ya Somalia iliyotolewa Jumatatu wiki hii inaonyesha dalili dhahiri kwamba njaa itatokea katika maeneo mawili ya Mkoa wa Bay (wilaya za Baidoa na Burhakaba) Kusini-Kati mwa Somalia kati ya Oktoba na Desemba.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kukiwa na misimu mitano mfululizo ya mvua duni, kupungua kwa uwezo wa kustahimili kwa jamii zilizoathiriwa, kupungua kwa mali za kujikimu, na mambo mengine yanayozidisha hali mbaya, msaada wa kibinadamu utahitajika kushughulikia viwango vya juu vya mahitaji baada ya Desemba 2022.

"Narudia: Hili ni tahadhari ya mwisho kwetu sote. Hali na mienendo inafanana na ile iliyoonekana katika msukomsuko wa Mwaka 2010-2011. Isipokuwa kwa sasa ni mbaya zaidi," Griffiths amesema.

Ameeleza kuwa kunyesha mvua duni kwa misimu minne ya mvua mfululizo, miongo kadhaa ya migogoro, watu wengi kulazimika kuyahama makazi yao, na masuala makubwa ya kiuchumi yanawasukuma watu wengi kwenye hatari ya baa la njaa.

"Na hali hizi zinaweza kudumu hadi angalau Machi 2023," amesema, huku akionyesha kuwa Baidoa ni kitovu cha msukosuko wa kibinadamu nchini Somalia.

"Sio sehemu pekee yenye mahitaji, lakini ni mojawapo. Katika kambi za watu walioyakimbia makazi yao, tuliona njaa kali. Katika hospitali ya Baidoa, tulikuwa na fursa isiyoweza kuepukika ya kuona watoto wakiwa na utapiamlo kiasi kwamba hawakuweza kuzungumza." mkuu huyo wa misaada wa Umoja wa Mataifa amesema.

Umoja wa Mataifa ulisema Mkoa wa Bay pia ulikuwa kitovu cha mzozo wa kibinadamu Mwaka 2017 wakati ukame mkali ulisababisha jamii za wafugaji na wakulima na waliokimbia makazi kukabiliwa na hatari ya njaa, ambayo iliepukwa tu kutokana na msaada wa kibinadamu uliotolewa kwa wakati, nguvu na uendelevu.

Griffiths amesema watoto milioni 1.5 kote nchini Somalia watakabiliwa na utapiamlo wa hali ya juu ifikapo Oktoba mwaka huu ikiwa hali itaendelea kama ilivyo sasa. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha