Waziri Mkuu wa China akutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Tanzania

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 04, 2022
Waziri Mkuu wa China akutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Tanzania
Waziri Mkuu wa China Li Keqiang akikutana na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anayezuru China kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing, China, Novemba 3, 2022. (Xinhua/Zhai Jianlan)

BEIJING - Waziri Mkuu wa China Li Keqiang amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anayezuru Beijing siku ya Alhamisi.

Akipongeza maendeleo ya uhusiano kati ya China na Tanzania, Li amesema Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China umefanya mipango mkakati kwa ajili ya maendeleo ya China katika kipindi kijacho, na China itaendelea kusukuma mbele kufungua mlango kwenye kiwango cha juu.

Li amesema China iko tayari kushirikiana na Tanzania ili kuongeza kushabihiana kwa mikakati ya maendeleo, kuimarisha ushirikiano katika sekta muhimu kama vile uchumi na biashara, nishati, afya, kilimo na uvuvi, na kuboresha mabadilishano kati ya watu wa nchi hizo mbili.

“China iko tayari kupanua uagizaji wa bidhaa za Tanzania zinazokidhi kuingia sokoni na kuhimiza makampuni ya China kuongeza uwekezaji nchini Tanzania,” amesema Li, na kuongeza kuwa upande wa China unatumai kuwa Tanzania itatoa uungaji mkono unaohitajika.

Kuhusu uhusiano wa China na Afrika, Li amesema China inapenda kushirikiana na nchi za Afrika kwenye msingi wa ukweli na usawa, kuongeza mshikamano na kuaminiana, na kutafuta maendeleo jumuishi na endelevu.

Kwa upande wake, Rais Hassan ameishukuru China kwa uungaji mkono na msaada wake kwa Tanzania kwa miaka mingi, akisema Tanzania inashikilia kithabiti sera ya kuwepo kwa China moja na imejitolea kuendeleza urafiki wake wa jadi na China.

Amesema Tanzania itatekeleza matokeo ya Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika, kuhimiza ushirikiano katika masuala ya biashara, uwekezaji, kilimo, uvuvi, miundombinu na mabadilishano kati ya watu na watu.

“Tanzania inakaribisha uwekezaji kutoka kwa makampuni ya China,” Samia ameongeza.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha