Kampuni ya Teknolojia ya China Huawei yazindua mfuko wa kuendeleza viongozi wa uvumbuzi nchini Zambia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 04, 2022
Kampuni ya Teknolojia ya China Huawei yazindua mfuko wa kuendeleza viongozi wa uvumbuzi nchini Zambia
Kaimu Waziri wa Elimu wa Zambia Elijah Muchima akitoa hotuba kwenye uzinduzi wa mfuko wa teknolojia ya mawasiliano (TEHAMA) mjini Lusaka, Zambia, Novemba 3, 2022. Kampuni kubwa ya mawasiliano ya China Huawei Alhamisi imezindua mfuko wa teknolojia ya mawasiliano (TEHAMA) kuendeleza viongozi wa uvumbuzi ili kuharakisha ajenda ya mabadiliko ya kidijitali ya Zambia. (Xinhua/Martin Mbangweta)

LUSAKA, - Kampuni kubwa ya mawasiliano ya China Huawei Alhamisi imezindua mfuko wa teknolojia ya mawasiliano (TEHAMA) kuendeleza viongozi wa uvumbuzi ili kuharakisha ajenda ya mabadiliko ya kidijitali ya Zambia.

Mfuko huo unaoitwa Mfumo wa Uvumbuzi wa Hakainde Hichilema (Hakainde Hichilema Innovation Fund), ni sehemu ya ushirikiano na mpango wa miaka minne wa Huawei ambao utatoa mafunzo ya TEHAMA kwa vijana 5,000 ifikapo Mwaka 2025.

Makamu Mkuu wa Huawei Kanda ya Kusini mwa Afrika, Phil Li amesema kampuni hiyo inataka kusaidia kutambua na kuendeleza vipaji maalum na vinavyoweza kutegemewa ambavyo vinasisitiza ajenda ya mabadiliko ya kidijitali ya Zambia ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia TEHAMA.

"Ni nia yetu kutoa mafunzo ya msingi ya TEHAMA kwa angalau wakufunzi 50 na maafisa 50 wa serikali waliochaguliwa katika Wizara ya Elimu na washirika wake," amesema.

Kwa mujibu wake, uzinduzi huo unafuatia kutiwa saini kwa mkataba wa makubaliano kati ya Huawei na serikali mwezi Machi mwaka huu kwa ajili ya mpango wa uongozi wa uvumbuzi wa kidijitali.

Kampuni hiyo, imesema, pia itaanzisha kitovu cha uvumbuzi, eneo kwa ajili ya kuzalisha na kulea vipaji vya uvumbuzi na ukamilishaji wa mawazo ya TEHAMA ambayo yatashughulikia miundombinu yote muhimu inayohitajika kwa wabunifu kuzalisha, kuendeleza na kupima uwezekano wa ufumbuzi wao wa kidijitali chini ya ushauri makini wa wataalam waliojitolea.

Waziri wa Teknolojia na Sayansi wa Zambia Felix Mutati amekaribisha mpango huo na kuishukuru kampuni hiyo ya China akisema utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukuza ujuzi wa kidijitali na ujasiriamali miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya ufundi.

Katika hotuba yake iliyosomwa kwa ajili yake na katibu mkuu wa wizara hiyo Brilliant Habeenzu, waziri huyo ameipongeza Huawei kwa kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta ya TEHAMA nchini Zambia na kuendelea kuiunga mkono Zambia katika maendeleo ya sekta hiyo.

“Serikali imejitolea kufungua uwezo wa kiuchumi wa nchi kupitia TEHAMA,” amesema.

Kaimu Waziri wa Elimu wa Zambia, Elijah Muchima amesema serikali imeshirikiana na Huawei kuhakikisha kila mwanafunzi nchini humo anapata ujuzi wa kidijitali na kujiandaa kukabiliana na ulimwengu wa kidijitali unaobadilika kwa kasi.

Hata hivyo, amesema mapungufu bado yapo katika ujuzi wa kidijitali na ujasiriamali wa kidijitali na kuipongeza Huawei kwa kuja na mpango huo wa kuwapatia vijana ujuzi wa TEHAMA.

"Wizara yangu inaamini kwamba kupitia teknolojia na mifumo ya kidijitali, tunaweza kupeleka rasilimali za kujifunza katika maeneo yote ya nchi hii ili kila mwanafunzi nchini Zambia awe na ujuzi wa kidijitali kufungua uwezo wake," amesema.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha