Wapalestina waadhimisha miaka 18 ya kifo cha Marehemu Arafat

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 11, 2022
Wapalestina waadhimisha miaka 18 ya kifo cha Marehemu Arafat
Watu wa Palestina wakishiriki madhimisho ya miaka 18 tangu kutokea kifo cha kiongozi wa Palestina Marehemu Yasser Arafat katika Mji wa Gaza, Novemba 10, 2022. Wapalestina Alhamisi wameadhimisha miaka 18 ya kifo cha kiongozi wa Palestina Marehemu Yasser Arafat. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua)

GAZA/RAMALLAH - Wapalestina Alhamisi wameadhimisha miaka 18 tangu kutokea kifo cha kiongozi wa Palestina Marehemu Yasser Arafat.

Katika ukingo wa pwani wa Ukanda wa Gaza, makumi ya maelfu ya wakaazi wa eneo hilo walishiriki maandamano kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano baada ya kuondolewa kwa marufuku na chama tawala cha Palestinian Islamic Resistance Movement (Hamas).

Washiriki wengi walinyanyua bendera za Palestina na chama cha Fatah, huku wakiwa wamebeba picha kubwa za Arafat na kutamka kaulimbiu na nyimbo ambazo zilimpa heshima ya "cheche ya mapinduzi ya Palestina."

Akiwa ni mwanzilishi wa Fatah, mwenyekiti wa zamani wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Taifa la Palestina, Arafat amekuwa akiheshimiwa na Wapalestina wengi kama kielelezo cha matarajio yao ya kitaifa.

Wakati wa shughuli hiyo, Rais wa Palestina Mahmoud Abbas alisema katika hotuba yake iliyorekodiwa kwamba Arafat ameacha "urithi tajiri wa kitaifa kwa ajili yetu ambao sote tunapaswa kuuhifadhi na kuuendeleza."

Abbas ameapa kwamba harakati zake zitafuata njia sawa na za Arafat, huku akisisitiza kwamba PLO inayoongozwa na Fatah itaenedelea kuwa mwakilishi halali wa watu wa Palestina.

"Mgawanyiko wa ndani na Hamas umechukua hatua yetu nyuma ... na unatishia kupoteza mafanikio yaliyopatikana na watu wa Palestina, ambayo gharama yake ilikuwa kafara kubwa za waliojitolea muhanga, wafungwa na waliojeruhiwa," Abbas amesema.

Ameongeza kuwa Wapalestina hawatakubali kitu kingine zaidi ya kuwa na nchi huru ya Palestina kwenye mipaka ya Mwaka 1967, na Jerusalem Mashariki ikiwa ni mji mkuu wake.

Abbas pia ametoa wito kwa Wapalestina kujiandaa kwa hatua inayofuata "kuzuia mipango ya Israel ya unyakuzi wa ardhi kama tulivyowashinda hapo awali."

Naye Amed Helles, afisa mkuu wa Fatah huko Gaza, amesisitiza umuhimu wa kurejesha maridhiano kati ya makundi ya kisiasa ya Palestina haraka iwezekanavyo, ili kuandaa uchaguzi wa kidemokrasia na kutengeneza maisha ya kufaa kwa vizazi vipya vinavyostahili kuishi kwa heshima.

Novemba 11, 2004, Arafat alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 75 katika hospitali ya kijeshi karibu na Paris, Ufaransa kutokana na ugonjwa usiojulikana.

Mabaki ya mwili wa Arafat yalifukuliwa Novemba 2012 ili kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi, ambapo dutu ya polonium ilipatikana baada ya majaribio ya wanasayansi wa Ufaransa, Uswizi na Russia.

Mke wa Arafat alifungua keshi kwenye mahakama ya Ufaransa akitaka uchunguzi wa kifo cha mumewe. Hata hivyo, Mwezi Septemba, Mwaka 2015, majaji wa Ufaransa waliokuwa wakichunguza madai hayo walifunga kesi hiyo bila kufungua mashtaka yoyote. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha