Marais Xi Jinping na Joe Biden wafanya mazungumzo yenye uwazi na ya kina kuhusu uhusiano wa nchi mbili na masuala makubwa ya kimataifa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 15, 2022
Marais Xi Jinping na Joe Biden wafanya mazungumzo yenye uwazi na ya kina kuhusu uhusiano wa nchi mbili na masuala makubwa ya kimataifa
Rais wa China Xi Jinping akikutana na Rais wa Marekani Joe Biden mjini Bali, Indonesia, Novemba 14, 2022. (Xinhua/Li Xueren)

BALI, Indonesia - Rais wa China Xi Jinping na mwenzake wa Marekani, Joe Biden, wamefanya mazungumzo ya wazi na ya kina Jumatatu kuhusu masuala muhimu ya kimkakati ya uhusiano kati ya China na Marekani na masuala makubwa ya kimataifa na kikanda.

Rais Xi ameeleza kuwa hali ya sasa ya uhusiano kati ya China na Marekani haiko katika maslahi ya kimsingi ya nchi hizo mbili na watu wao, na si kile jumuiya ya kimataifa inachotarajia.

China na Marekani zinahitaji kuwa na hisia ya kuwajibika kwa historia, kwa Dunia na kwa watu, kuchunguza njia sahihi ya kuishi pamoja katika zama mpya, kuweka uhusiano kwenye mkondo sahihi, na kuurudisha kwenye mwelekeo wa ukuaji wenye tija na utulivu kwa manufaa ya nchi hizo mbili na Dunia kwa ujumla, Xi amesema.

Xi amezungumzia Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na matokeo yake muhimu, na kusema kwamba sera za ndani na nje za CPC na serikali ya China ziko wazi na zenye uwazi, na nia dhahiri ya kimkakati iliyotamkwa wazi yenye mwendelezo mkubwa na utulivu.

“China inasonga mbele na ustawishaji wa Taifa la China katika sekta zote kupitia njia ya Maendeleo ya Kisasa ya China, kwa kuzingatia juhudi zetu katika lengo la kukidhi matarajio ya watu ya maisha bora, kutafuta bila kuyumbayumba mageuzi na kufungua mlango, na kuhimiza ujenzi wa uchumi wa Dunia ulio wazi” Xi amesema.

Amesema China ina nia ya kuimarisha na kupanua ushirikiano wa kimataifa, kulinda mfumo wa kimataifa na Umoja wa Mataifa ukiwa msingi wake na utaratibu wa kimataifa unaoungwa mkono na sheria za kimataifa, na kujenga jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.

Ameongeza kuwa China itaendelea kujitolea kwa maendeleo ya amani, maendeleo ya kufungua mlango na maendeleo yenye manufaa kwa pande zote, kushiriki na kuchangia maendeleo ya kimataifa, na kutafuta maendeleo ya pamoja na nchi duniani kote.

Huku akiweka bayana kuwa Dunia iko katika hatua kubwa ya mabadiliko katika historia, Xi amesema kuwa nchi zinahitaji kukabiliana na changamoto ambazo hazijawahi kushuhudiwa na kutumia fursa ambazo hazijawahi kutokea, akiongeza kuwa huu ndiyo muktadha mkubwa zaidi ambao pande hizo mbili zinapaswa kutazama na kushughulikia uhusiano wa China na Marekani.

Xi pia ametoa maelezo kamili ya asili ya suala la Taiwan na msimamo wa kanuni ya kuwepo kwa China moja. Amesisitiza kuwa suala la Taiwan ndilo kiini cha maslahi ya China, msingi wa kisiasa wa uhusiano kati ya China na Marekani, na mstari mwekundu wa kwanza ambao haupaswi kuvukwa nchini ya uhusiano kati ya China na Marekani.

Kwa upande wake Biden amesema kuwa amemfahamu Rais Xi kwa miaka mingi na kudumisha mawasiliano ya mara kwa mara, lakini hakuna kitu kinachoweza kuchukua nafasi ya mkutano wao huo wa ana kwa ana.

Pamoja na kumpongeza Rais Xi kwa kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya CPC, Biden amesema upande wa Marekani umejitolea kuweka njia za mawasiliano wazi kati ya marais hao wawili na katika ngazi zote za serikali, ili kuruhusu mazungumzo ya wazi juu ya masuala ambayo pande hizo mbili hazikubaliani, na kuimarisha ushirikiano unaohitajika na kuchukua nafasi muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula na changamoto nyingine muhimu za kimataifa, ambazo ni muhimu sana kwa nchi hizo mbili na watu, na pia muhimu sana kwa Dunia nzima.

Biden amesisitiza tena kuwa China yenye utulivu na ustawi ni nzuri kwa Marekani na Dunia, na kwamba Marekani haitafuti vita baridi vipya. Pia amesisitiza kuwa Sera ya Marekani kuhusu Taiwan haijabadilika na Marekani inatambua uwepo wa China moja. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha