Watu 162 watangazwa kufariki Dunia wakati tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 5.6 likiikumba Indonesia (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 22, 2022
Watu 162 watangazwa kufariki Dunia wakati tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 5.6 likiikumba Indonesia
Watu walioathiriwa na tetemeko la ardhi wakiwa wamepumzika nje huko Cianjur, Java Magharibi, Indonesia, Novemba 22, 2022. Jumla ya watu 162 wameuawa baada ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 5.6 katika kipimo cha Richter kupiga Jimbo la Java Magharibi nchini Indonesia siku ya Jumatatu, maafisa wamesema. (Xinhua/Xu Qin)

JAKARTA - Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 5.6 katika kipimo cha Richter limekumba Jimbo la Magharibi mwa Indonesia la Java Magharibi siku ya Jumatatu, huku mitetemo ya tetemeko hilo ikihisiwa sana katika mji mkuu wa nchi hiyo, Jakarta na kuzua hofu, shirika la hali ya hewa, tabianchi na fizikia la Indonesia limesema.

Tetemeko hilo lilitokea saa 7:21 Mchana saa za Jakarta (0621 GMT) huku kitovu kikuu cha tetemeko kikiwa umbali wa kilomita 10 Kusini Magharibi mwa Wilaya ya Cianjur katika Jimbo la Java Magharibi, na kina cha kilomita 10 chini ya ardhi, shirika hilo limesema.

Taarifa zinasema kuwa hadi kufikia Jumatatu jioni kwa saa za huko jumla ya watu 162 walikuwa wamefariki.

Tetemeko hilo pia limesababisha uharibifu mkubwa kwa nyumba nyingi, majengo na miundombinu. Mitetemo ya tetemeko hilo imehisiwa sana katika mji mkuu wa nchi hiyo, Jakarta.

Takribani watu 13,784 wamelazimika kuyakimbia makazi yao na kujihifadhi kutokana na nyumba zao kuharibiwa na tetemeko hilo, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wakala wa kudhibiti na kukabiliana na maafa wa Wilaya ya Cianjur, mojawapo ya maeneo yaliyoathirika zaidi.

Miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko hilo ni pamoja na barabara, daraja, majengo ya shule, majengo ya ofisi, misikiti na vituo vya afya, imesema.

“Ongezeko kubwa la idadi ya waliopoteza maisha limetokana na ripoti mpya ya maporomoko ya ardhi yaliyofunika wakazi wapatao 100”, Nena Fatimah, Afisa Mkuu katika kitengo cha data na habari cha wakala wa usimamizi na udhibiti wa maafa wa wilaya hiyo, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwa njia ya simu.

Shirika hilo limeanzisha vituo 47 vinavyotoa misaada ikiwa ni pamoja na vyakula na dawa kwa waathiriwa wa tetemeko hilo, kwa mujibu wa msemaji wa Shirika la Taifa la Kukabiliana na Majanga, Abdul Muhari.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha