OECD yakadiria ukuaji wa uchumi duniani kupungua hadi asilimia 2.2 Mwaka 2023 (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 23, 2022
OECD yakadiria ukuaji wa uchumi duniani kupungua hadi asilimia 2.2 Mwaka 2023
Picha iliyopigwa Februari 17, 2022 ikionyesha mandhari ya jiji la Singapore. (Picha na Then Chih Wey/Xinhua)

PARIS - Ukuaji wa Pato la Jumla duniani (GDP) unatarajiwa kushuka kutoka asilimia 3.1 mwaka huu hadi asilimia 2.2 Mwaka 2023, Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) limesema katika ripoti yake mpya ya Mtazamo wa Uchumi siku ya Jumanne.

Kiwango hicho cha ukuaji cha Mwaka 2022 ni karibu nusu ya kasi iliyorekodiwa Mwaka 2021 wakati wa uchumi kuimarika kutoka kwenye janga la UVIKO-19, na kiwango cha ukuaji kinachotarajiwa Mwaka 2023 ni chini ya kile kilichokadiriwa kabla ya kuzuka kwa mgogoro kati ya Russia na Ukraine.

"Asia itakuwa injini kuu ya ukuaji uchumi katika Mwaka 2023 na 2024, ambapo Ulaya, Amerika Kaskazini na Amerika Kusini zitashuhudia ukuaji wa chini sana," imesema ripoti hiyo.

Masoko makubwa yanayoibukia barani Asia yanakadiriwa na OECD kuchangia karibu robo tatu ya ukuaji wa Pato la Jumla Duniani Mwaka 2023, huku uchumi wa Marekani na Ulaya ukitarajiwa kupungua.

"Ukitatizwa na bei ya juu ya nishati na chakula, imani dhaifu, kuendelea kwa vikwazo vya ugavi na athari za awali za sera kali ya fedha, ukuaji wa uchumi wa kila mwaka katika eneo la euro Mwaka 2023 unatarajiwa kuwa asilimia 0.5," shirika hilo limesema.

Uchumi wa Marekani utakua tu kwa asilimia 0.5 Mwaka 2023, ikilinganishwa na asilimia 1.8 Mwaka 2022.

Masoko ya nishati yanabakia kuwa kati ya hatari kubwa za kushusha chini ukuaji wa uchumi.

"Ulaya imepiga hatua kubwa kujaza akiba yake ya gesi asilia na kupunguza mahitaji, lakini msimu huu wa baridi katika Ulimwengu wa Kaskazini utakuwa na changamoto," imesema ripoti, na kuongeza kuwa bei ya juu ya gesi au usumbufu wa usambazaji wa gesi utasababisha ukuaji dhaifu wa uchumi na mfumuko wa bei barani Ulaya na duniani Mwaka 2023 na 2024.

Kuongeza kasi ya uwekezaji katika kuhamia na kuendeleza vyanzo na teknolojia ya nishati safi itakuwa muhimu kwa usambazaji wa nishati mbalimbali na kuhakikisha usalama wa nishati, OECD imesisitiza. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha