Kiwanda cha nguo cha China chahimiza maendeleo ya mji mdogo wa Ethiopia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 25, 2022
Kiwanda cha nguo cha China chahimiza maendeleo ya mji mdogo wa Ethiopia
Tarehe 16, Novemba, Mwaka 2022, wafanyakazi wenyeji wakifanya kazi katika kiwanda cha kuchapa na kutia rangi kwenye vitambaa cha Kampuni ya Nguo ya Mina ya Zhejiang huko Sebeta, Ethiopia. (Xinhua/Michael Tewelde)

Tangu kuanzishwa kwa Kiwanda cha Nguo cha China, Worku Lemi ameshuhudia mabadiliko makubwa katika maisha yake na mji wake.

Sebeta iliyoko kwenye eneo la Oromia lenye umbali wa maili kadhaa kutoka Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, ulikuwa mji wa wilaya ya kilimo hapo zamani, lakini kuanzishwa kwa Kampuni ya Nguo ya Mina ya Zhejiang kumesaidia kuleta mabadiliko ya kufurahisha kwa mji huo wa Ethiopia na maisha ya wakaazi wa eneo hilo.

Kiwanda hicho cha kuchapa na kutia rangi vitambaa chenye mashine za chapa za kimataifa, sasa kina uwezo wa kutengeneza mita 200,000 za vitambaa vilivyochapwa maua na kutiwa rangi kwa siku, na bidhaa zake zinauzwa kwenye masoko ya Ulaya na ya ndani na nchi jirani za Afrika.

Lemi mwenye umri wa miaka 31 ni mhitimu wa kozi ya uhasibu, alijiunga na Kiwanda cha Nguo cha Arbaminch ya Kampuni ya Nguo ya Mina ya Zhejiang miaka saba iliyopita.

"Kabla ya kuwa msimamizi, nilikuwa msaidizi wa mwendeshaji mashine wa China. Nimejifunza mengi kutoka kwake," Lemi alisema. Alihusisha ukuaji wake na utaratibu mzuri wa kubadilishana uzoefu kati ya wataalamu wa China na Ethiopia.

"Watu karibu 300 wanafanya kazi hapa. Ninawashukuru sana wawekezaji wa China kwa kutuletea nafasi hii ya thamani kwetu," aliongeza.

Mkuu wa uendeshaji na uuzaji wa kampuni hiyo, Abdurhaman Kemal alisifu mashine za kisasa za kiwanda hicho na utaratibu mpya wa kazi, ambavyo vimefanya kazi ya kimapinduzi katika sekta ya viwanda vya nguo nchini Ethiopia.

Akizingatia kuongezeka kwa idadi ya vijana wa Ethiopia wanaohitimu kutoka vyuo vikuu mbalimbali na vituo vya elimu na mafunzo ya ufundi wa kazi, Kemal alisisitiza umuhimu wa kiwanda katika kutoa nafasi za ajira na kutoa nafasi za utafiti wa teknolojia kwa msaada wa maabara zake za kisasa.

"Mbali na juhudi kubwa za kuhamisha ujuzi na maarifa, wataalam wa ufundi wa China pia wanawezesha wafanyakazi wetu wenyeji kunufaika pamoja na utamaduni wao wa kufanya kazi kwa bidii " alisema.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha