Zaidi ya wahamiaji haramu 200 warudishwa katika nchi zao kutoka Libya (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 25, 2022
Zaidi ya wahamiaji haramu 200 warudishwa katika nchi zao kutoka Libya
Wahamiaji haramu wakisubiri kuondoka katika Ofisi ya Uhamisho ya Idara ya Kupambana na Uhamiaji Haramu huko Tripoli, Libya, Novemba 24, 2022. (Picha na Hamza Turkia/Xinhua)

TRIPOLI - Idara ya Kupambana na Uhamiaji Haramu ya Libya Alhamisi iliwarudisha zaidi ya wahamiaji haramu 200 katika nchi zao.

Kwa mujibu wa Nasser al-Khatroushi, Mkuu wa Ofisi ya Uhamisho ya Idara ya Kupambana na Uhamiaji haramu ya Libya, wahamiaji hao ambao wanatoka Misri, Niger na Sudan, wamerudishwa katika nchi zao kupitia safari za barabara.

Urudishaji huo makwao wa wahamiaji haramu umefanyika kwa mara ya kwanza kwa ushirikiano wa Idara za Kupambana na Uhamiaji haramu za Mashariki na Kusini mwa Libya, afisa wa Libya ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.

"Leo, tuna furaha kubwa kuona maafisa kutoka Magharibi, Mashariki na Kusini mwa Libya wamekusanyika hapa Tripoli kutatua suala la uhamiaji haramu, ambalo ni suala gumu," amesema Mohamed al-Khoja, Mkuu wa Idara ya Kupambana na Uhamiaji haramu ya Libya.

Libya imekuwa sehemu inayopendelewa zaidi kwa wahamiaji haramu wanaojaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kufika pwani za Ulaya.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), jumla ya wahamiaji haramu 20,842 wakiwemo wanawake na watoto wameokolewa baharini na kurejea Libya hadi sasa mwaka huu.

Wakati huo huo, wahamiaji haramu 500 wamekufa na wengine 863 hawajulikani walipo kwenye pwani ya Libya katika njia ya Kati ya Mediterania, IOM imesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha