Anwar Ibrahim aapishwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Malaysia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 25, 2022
Anwar Ibrahim aapishwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Malaysia
Waziri Mkuu mteule wa Malaysia Anwar Ibrahim akiondoka baada ya mkutano na waandishi wa habari kufuatia hafla za kuapishwa kwake huko Selangor, Malaysia, Novemba 24, 2022. Anwar Ibrahim, naibu waziri mkuu wa zamani, amekula kiapo siku ya Alhamisi na kuwa waziri mkuu mpya wa Malaysia. (Xinhua/Zhu Wei)

KUALA LUMPUR - Anwar Ibrahim, naibu waziri mkuu wa zamani, amekula kiapo siku ya Alhamisi na kuwa waziri mkuu mpya wa Malaysia.

Anwar, ambaye anaongoza muungano wa vyama vya kisiasa wa Pakatan Harapan (PH), alionekana akiwa amevalia mavazi ya kitamaduni ya Kimalay na kuahidi kuitumikia Malaysia na watu vyema mbele ya Mfalme wa Malaysia Sultan Abdullah Sultan Ahmad Shah kwenye ikulu ya taifa katika matangazo ya moja kwa moja ya vyombo vya habari.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na washirika wa kisiasa wa Anwar.

Anwar mwenye umri wa miaka 75, amewahi kuwa naibu waziri mkuu chini ya waziri mkuu wa zamani Mahathir Mohamad kutoka Mwaka 1993 hadi 1998 katika serikali ya Barisan Nasional (BN). Kufuatia kutofautiana na Mahathir, Anwar baadaye aliunda Chama cha Haki cha Umma, maarufu kwa kifupi chake cha Kimalay PKR na baadaye kugombea katika chaguzi kadhaa za kitaifa.

Katika safari yake ya kisiasa akiwa BN amewahi pia kushikilia nyadhifa za vijana na michezo, elimu, kilimo na fedha.

Chama cha PKR baadaye kiliunda muungano wa PH na vyama vingine kadhaa vya upinzani, huku muungano huo ukishinda uchaguzi mkuu Mwaka 2018, na kumaliza utawala wa muda mrefu wa Chama cha BN ambacho kilichukua mamlaka kutoka kipindi Malaysia ilijipatia uhuru hadi Mwaka 2018.

Anwar amesema lengo la msingi la serikali yake litakuwa kufufua uchumi, utulivu wa kisiasa na kuhakikisha uhusiano mzuri baina ya jamii kati ya makabila na dini mbalimbali katika nchi hiyo.

"Hii ni serikali ya umoja wa kitaifa, nyote mnakaribishwa mradi tu kukubali kupambana na ufisadi, kuwa na utawala bora, na Malaysia kwa Wamalaysia wote," ameuambia mkutano na waandishi wa habari Alhamisi usiku kufuatia hafla ya kuapishwa kwake.

Anwar ameahidi kuelekeza nguvu zake katika vita dhidi ya kile alichokiita rushwa iliyokithiri pamoja na kuhakikisha utawala bora, mahakama huru na ustawi wa watu.

Akiitaja China kuwa jirani muhimu, waziri mkuu huyo mpya amesema serikali yake itatoa kipaumbele katika kuimarisha uhusiano na China katika nyanja za biashara, uwekezaji na utamaduni.

“Kwa manufaa ya maslahi ya kiuchumi ya watu wa Malaysia, nafasi ya China ni muhimu,” amesema.

Ameeleza kuwa, ameagiza chama chake kuandaa utaratibu wa kura ya imani ili kupima kukubalika na kuungwa mkono kwake kwa wingi wakati bunge litakapokutana tena Desemba 19, baada ya wapinzani wake wa kisiasa kupinga kukubalika kwake kwa wingi.

Malaysia ilikuwa katika mkwamo wa kisiasa kufuatia matokeo ya uchaguzi wa Jumamosi iliyopita ambayo hayakuamua mshindi, bila muungano wowote wa kisiasa au chama kilichopata viti vya kutosha katika Baraza la Chini la Bungili kuunda serikali peke yake.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha