

Lugha Nyingine
Morocco yavuta hisia za soka duniani kwa kuichapa Ubelgiji katika siku ya michezo ya Kombe la Dunia iliyojaa mishangao (2)
DOHA – Mishangao imeendelea siku ya nane ya Kombe la Dunia la FIFA 2022 siku ya Jumapili huku Morocco ikipata ushindi wake wa kwanza katika kipindi cha miaka 24 kwenye michuano hiyo kwa kuichapa Ubelgiji 2-0.
Ushindi wa mwisho wa timu hiyo ya Afrika katika mechi za Kombe la Dunia ilikuwa Mwaka 1998 walipoifunga Scotland mabao 3-0 mjini Saint-Etienne, Ufaransa.
Huo ulikuwa ushindi wa tatu pekee kwa Morocco katika historia ya Kombe la Dunia, wa kwanza ulikuwa Mwaka 1986 kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ureno.
Vijana wa Kocha Walid Regragui walitikisa nyavu dakika ya 73 baada ya Abdelhamid Sabiri ambaye alikuwa tu ameingia uwanjani kupiga mpira wa faulo ambao Romain Saiss aliweza tu kuugusa kidogo kuuweka wavuni.
Zakaria Aboukhlal aliweka matokeo katika uhakika wa ushindi kwa kufyatua shuti kwenye paa la wavu dakika za lala salama baada ya mkwaju wa Hakim Ziyech.
Katika uwanja wa Ahmad Bin Ali, Costa Rica ilifufuka kutoka kwenye kichapo cha aibu katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Hispania na kushinda Japan 1-0.
Beki wa kulia Keysher Fuller alifunga dakika ya 81 kwa timu hiyo ya Amerika ya Kati baada ya kupewa pasi na Yeltsin Tejeda.
“Ikilinganishwa na mimi mwenyewe kufunga bao, ni muhimu zaidi kuipeleka timu kupata ushindi na kuweka matumaini yetu ya kusonga mbele katika hatua ya mtoano,” amesema Fuller.
Katika Uwanja wa Kimataifa wa Khalifa, Andrej Kramaric aliifungia mabao mawili Croatia ikitoka nyuma na kuwalaza Canada 4-1, matokeo ambayo yalivunja matumaini ya Kocha Maple Leafs kutinga hatua ya mtoano.
Alphonso Davies wa Bayern Munich aliipatia Canada bao la kuongoza kwa kichwa dakika ya pili, kabla ya Kramaric na Marko Livaja kufunga ndani ya dakika nane na kuwapa Croatia bao la kuongoza kabla ya kipindi cha mapumziko.
Canada, inayocheza Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu Mwaka 1986, ilijiunga na wenyeji Qatar ambayo ilikiwa timu za kwanza kuondolewa kwenye michuano hiyo.
Katika mechi ya mwisho ya Jumapili, Niclas Fullkrug aliyetokea benchi alifunga bao dakika ya 83 na kuifanya Ujerumani iambulie sare ya 1-1 dhidi ya Hispania.
Alvaro Morata aliifungia Hispania bao la kuongoza dakika ya 62 kwa shuti la mguu kutoka eneo la hatari baada ya pasi ya Jordi Alba.
Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea leo Jumatatu kwa michezo ya Kundi G ambapo mwakilishi wa Afrika, Cameroon itamenyana na Serbia wakati Brazil itavaana na Switzerland. Pia kutakuwa na michezo ya Kundi H ambapo Korea Kusini itapambana na mwakilishi mwingine wa Afrika, Ghana. Mchezo mwingine katika kundi hilo utakuwa kati ya Ureno na Uruguay.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma