China yawatangaza wanaanga wa Chombo cha Shenzhou-15 kwa ajili ya safari kwenye kituo cha anga ya juu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 29, 2022
China yawatangaza wanaanga wa Chombo cha Shenzhou-15 kwa ajili ya safari kwenye kituo cha anga ya juu
Picha hii isiyo na tarehe ikimuonyesha Fei Junlong, mmoja wa wanaanga watatu ambao watashiriki kwenye safari ya anga ya juu ya Chombo cha Shenzhou-15. Wanaanga wa China Fei Junlong, Deng Qingming na Zhang Lu wametangazwa kushiriki misheni ya anga ya juu kutekeleza majukumu kwenye chombo cha Shenzhou-15, na Fei atakuwa kamanda, Shirika la Anga ya Juu la China (CMSA) limetangaza katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu. (Xinhua)

JIUQUAN - Wanaanga wa China Fei Junlong, Deng Qingming na Zhang Lu wametangazwa kuwa watashiriki safari ya anga ya juu kwenye chombo cha Shenzhou-15, na Fei atakuwa kamanda, Shirika la Anga ya Juu la China (CMSA) limetangaza katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu.

Fei amewahi kushiriki katika misheni ya anga ya juu kwenye Chombo cha Shenzhou-6 na wote Deng na Zhang ni mara ya kwanza kwao kufanya safari kwenye anga ya juu, kwa mujibu wa Ji Qiming, msaidizi wa mkurugenzi wa CMSA.

"Ninajivunia sana kuwa kwenye misheni tena. Ninafuraha sana kuwekwa katika kituo cha anga ya juu cha China. Ninajivunia nchi yangu kuu," amesema Fei alipokutana na waandishi wa habari kuzungumzia misheni ijayo.

Deng, ambaye ni mmoja wa wanaanga 14 wa kwanza waliofunzwa nchini China miaka 24 iliyopita, amewahi kutoa msaada kwa safari kadhaa za chombo cha anga ya juu kama mbadala. "Nitafurahia fursa hii ya kuruka angani na kutimiza wajibu wangu," amesema Deng kwenye mkutano na wanahabari.

Zhang alichaguliwa kuwa mmoja wa kundi la pili la wanaanga wa China miaka 12 iliyopita. "Niko tayari kwa safari yangu ya kwanza kwenye anga ya juu," amesema. "Nitaruka kwa ajili ya ndoto yangu ya kibinafsi na kwa ajili ya ndoto ya taifa letu."

Akizungumzia kuhusu makabidhiano ya kazi yanayokuja na wanaanga wa Chombo cha Shenzhou-14, Zhang amesema "tuna zawadi kwa ajili yao, lakini tutaiweka siri kwa sasa."

Misheni hii ya wanaanga watatu ya chombo cha Shenzhou-15 itakuwa ya sita ya mpango wa anga ya juu wa China mwaka huu na ya mwisho katika awamu ya ujenzi wa kituo cha anga ya juu cha China, amesema Ji. Pamoja na wanaanga hao wa Shenzhou-15 kuwa angani hivi karibuni, kutakuwa na jumla ya wanaanga 12 kwenye misheni nne zinazofanya kazi katika ujenzi wa obiti wa kituo cha anga ya juu cha China.

Wakati wa kukaa kwao katika obiti, wanaanga hao wa Shenzhou-15 watazunguka na wanaanga watatu wa Shenzhou-14 katika obiti na kushuhudia kuwasili kwa chombo cha mizigo cha Tianzhou-6 na chombo cha anga ya juu ya Shenzhou-16. Pia watakuwa na makabidhiano ya kazi na wanaanga wa Shenzhou-16 katika obiti.

Chombo cha anga ya juu cha Shenzhou-15 kimepangwa kurushwa saa 11:08 jioni. Jumanne (Saa za Beijing) kutoka Kituo cha Urushaji Satelaiti cha Jiuquan Kaskazini-Magharibi mwa China. Urushaji huo utafanywa kwa roketi ya kubeba ya Long March-2F.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha