Rais Xi Jinping afanya mazungumzo na Rais wa Laos

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 01, 2022
Rais Xi Jinping afanya mazungumzo na Rais wa Laos
Xi Jinping, Katibu mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Rais wa China akiwa katika picha ya pamoja na Thongloun Sisoulith, Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi cha Laos na Rais wa Laos, kwenye Jumba Kuu la Mikutano ya Umma, Beijing, China, Novemba 30, 2022. (Xinhua/Rao Aimin)

BEIJING - Xi Jinping, Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Rais wa China, amefanya mazungumzo Jumatano na Thongloun Sisoulith, Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi cha Laos (LPRP) na Rais wa Laos.

Viongozi hao wawili wamesisitiza haja ya kushikilia kanuni ya "utulivu wa muda mrefu, urafiki wa ujirani mwema, kuaminiana na ushirikiano wa pande zote" na roho ya "majirani wema, marafiki, makomredi na washirika" katika kuendeleza uhusiano kati ya nchi mbili.

Nchi hizo mbili zitaheshimiana na kuaminiana kisiasa, kunufaishana kiuchumi, kuzidisha maelewano na upendo wa dhati katika mazungumzo kati ya watu wa pande mbili, kuzidisha ujenzi wa jumuiya ya China na Laos yenye mustakabali wa pamoja, na kuchangia ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja, kwa mujibu wa viongozi hao.

Mwanzoni mwa mazungumzo hayo, Xi alisema kuwa Komredi Jiang Zemin amefariki dunia siku ya Jumatano huko Shanghai kutokana na ugonjwa baada ya matibabu yote kushindwa.

Xi amesema Komredi Jiang alikuwa kiongozi bora mwenye heshima ya juu inayotambuliwa na Chama kizima, jeshi zima na watu wa China wa makabila yote, muumini mkubwa wa Umarx, mwanamapinduzi mkubwa wa wakulima, mwanasiasa, mwanamikakati wa kijeshi na mwanadiplomasia, mkomunisti aliyejaribiwa kwa muda mrefu, mpiganaji, na kiongozi bora wa lengo kuu la ujamaa wenye unaalum wa China. Xi amesema, Jiang alikuwa kiini cha kizazi cha tatu cha CPC cha uongozi wa pamoja na mwanzilishi mkuu wa Nadharia ya Uwakilishi Mtatu.

Kwa upande wake Thongloun pia ametoa salamu za rambirambi kwa kifo cha Komredi Jiang, akisema kuwa ni hasara kubwa kwa CPC na watu wa China, na LPRP na watu wa Laos wanahisi vivyo hivyo.

Thongloun amesema Chama, serikali na watu wa Laos watashirikiana na wenzao wa China ili kuendelea kusukuma mbele urafiki kati ya China na Laos.

Kuhusu uhusiano kati ya China na Laos, Xi amesema yuko tayari kushirikiana na Katibu Mkuu Thongloun kuendeleza ujenzi wa jumuiya ya China na Laos yenye mustakabali wa pamoja, huku akipongeza matokeo yenye matunda tangu kutiwa saini kwa mpango wa utekelezaji wa lengo hili Mwezi Aprili, Mwaka 2019.

Juu ya uhusiano wa kiuchumi na kibiashara, Xi amesema China itahimiza kampuni nyingi zaidi za China kuwekeza Laos na kukaribisha bidhaa bora zaidi kutoka Laos kuingia katika soko la China.

Ameongeza kuwa China iko tayari kuimarisha uratibu na ushirikiano kati yake na Laos ndani ya mifumo ya ushirikiano wa Lancang-Mekong na ushirikiano kati ya China na Jumuiya ya Nchi za Asia Kusini Mashariki (ASEAN).

Baada ya mazungumzo hayo, Xi na Thongloun kwa pamoja walishuhudia utiaji saini hati za ushirikiano kuhusu vyama vya siasa, uchumi na biashara, fedha, utamaduni na elimu na serikali za mitaa.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha