Makampuni ya China yafanya maonyesho ya nafasi za ajira kwa wanafunzi wa Kenya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 14, 2022
Makampuni ya China yafanya maonyesho ya nafasi za ajira kwa wanafunzi wa Kenya
Mwanafunzi (kushoto) akizungumza na mwakilishi wa kampuni kwenye maonyesho ya nafasi za ajira ya makampuni ya China huko Nairobi, Kenya, Desemba 13, 2022. Makampuni ya China yameanza maonyesho ya nafasi za ajira ya siku mbili Jumanne katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, na kutoa nafasi 300 za ajira kwa wanafunzi wa Kenya. (Xinhua/Li Yahui)

NAIROBI - Makampuni ya China yameanza maonyesho ya nafasi za ajira ya siku mbili Jumanne katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, na kutoa nafasi 300 za ajira kwa wanafunzi wa Kenya.

Maonesho hayo ya kuajiri yameandaliwa na Chuo cha Confucius katika Chuo Kikuu cha Nairobi kwa msaada wa makampuni 21 ya China yanayowekeza nchini Kenya.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Julius Ogeng'o, Naibu Chansela wa Masuala ya Kielimu katika Chuo Kikuu cha Nairobi, amesema maonyesho hayo ya nafasi za ajira yanatoa fursa kwa wanafunzi kuzungumza ana kwa ana na waajiri watarajiwa, na hivyo kuongeza uwezekano wa nafasi zao za kuajiriwa.

Amesema kampuni za China zimekuwa waajiri wazuri kwa sababu zina utamaduni wa kuhimiza uraia wa kimataifa miongoni mwa wafanyakazi wao wa nchi husika.

Wang Shangxue, Mkurugenzi wa China wa Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Nairobi, amesema zoezi hilo la kuajiri linawezesha makampuni ya China kuchagua wanafunzi bora zaidi wa Kenya.

Megan Muriuki, msimamizi katika Shirika la Usafirishaji Baharini la COSCO, amesema kampuni yake inashiriki katika maonyesho hayo ya nafasi za ajira huku ikitafuta kuajiri wafanyakazi wa ziada wa nchini humo ili kusaidia shughuli zao nchini Kenya.

"Tumechagua maonyesho ya nafasi za ajira ya Chuo Kikuu cha Nairobi kwa sababu yana wanafunzi wanaojua Lugha ya Kichina kwa ufasaha," ameongeza.

Sharon Simiyu, mwanafunzi wa Shahada ya Elimu katika chuo hicho, amesema maonyesho hayo ya nafasi za ajira yanatoa matarajio kwa wanafunzi wa Kenya kuajiriwa hata kabla ya kuhitimu. "Natumai kupata kazi katika eneo ninalopenda ili niweze kuimarisha ujuzi niliojifunza darasani."

Stephen Kamau Karanja, mwanafunzi wa Shahada ya Maendeleo ya Utotoni, amesema anashiriki katika maonyesho hayo ya nafasi za ajira kwa sababu anatumai ajira yake ya kwanza rasmi itakuwa na kampuni ya China.

"Nimekutana na Wachina mara kadhaa; kulingana na uzoefu huo, naweza kusema ni wazuri sana. Ningependa kufanya kazi nao," Karanja ameongeza.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha