Furaha kwa Messi, hat-trick ya kukatisha tamaa kwa Mbappe wakati Argentina ikishinda Fainali ya Kombe la Dunia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 19, 2022
Furaha kwa Messi, hat-trick ya kukatisha tamaa kwa Mbappe wakati Argentina ikishinda Fainali ya Kombe la Dunia
Lionel Messi (kati) wa Argentina akishangilia pamoja na wachezaji wenzake kwenye hafla ya kukabidhi Kombe la Dunia la FIFA 2022 katika Uwanja wa Lusail, Qatar, Desemba 18, 2022. (Xinhua/Cao Can)

DOHA - Argentina ndiyo bingwa wa Kombe la Dunia na Lionel Messi hatimaye ana taji ambalo limemponyoka kwa muda mrefu. Lakini wameweza kufanya hivyo kwa njia ngumu baada ya kile ambacho kitakuja kuhadithiwa kama moja ya fainali kubwa zaidi za Kombe la Dunia za wakati wote. Argentina waliongoza 2-0, lakini mabao mawili kutoka kwa Kylian Mbappe pekee ndani ya sekunde 100 yaliulazimisha mchezo kwenda muda wa ziada, ambapo Messi alifunga tena, Mbappe akaifungia tena Argentina na kufanya matokeo kuwa 3-3 katika dakika 120 za mchezo.

Katika mchezo huo, Emiliano Martinez alikuwa mwokozi, akiokoa mkwaju muhimu katika dakika za lala salama za muda wa ziada na kuokoa penati kwenye kipindi cha kupigiana mikwaju ya penati, na kuongeza jina lake kwenye orodha ya mashujaa wa Argentina.

Argentina walianza kwa nguvu, huku safu yao ya kiungo ikiwazidi ujanja Wafaransa, ambao walikuwa na wakati mgumu kuweza kutoka nje ya nusu yao.

Di Maria alifanya vyema zaidi katika dakika ya 21, akimgeukia Ousmane Dembele, ambaye baadaye alimkwatua kisigino na hivyo mwamuzi kutenga mkwaju wa penati iliyokwamishwa wavuni na Lionel Messi dakika ya 23 ya mchezo. Di Maria aliiandikia Argentina bao la pili dakika ya 36 na kuashiria furaha ya mapema ya kunyanyua kombe.

Hata hivyo Mbape aliyeonesha ujuzi na juhudi za aina yake katika mchezo huo alileta maajabu katika mchezo huo kwa kufunga magoli mawili ya kusawazisha ndani ya sekunde 100 tu, kwa bao la kwanza la penati dakika ya 80 na la kusawazisha dakika ya 81 hivyo kuufanya mchezo kwenda muda wa ziada.

Messi aliwatanguliza tena Argentina kwa bao la dakika ya 108 na kuonesha kama mwisho wa Ufaransa kufurukuta, hata hivyo ni Mbape tena aliyekata shangwe za Argentina kwa mkwaju wa penati uliompa hat trick ya mchezo mnano dakika ya 118 baada ya shuti lake kugonga mkono wa Gonzalo Montiel na refa kuelekeza kwenye penati.

Kolo Muani alipaswa kuwafungia Ufaransa goli la ushindi dakika za lala salama lakini mlindamlango Martinez aliweka mguu nje na kuokoa hatari wakati mshambuliaji huyo alipofika langoni.

Baada ya patashika na piga nikupige, mchezo huo uliamuliwa kwa matuta ya penati ambapo Argentina ilitia wavuni penati 4 na Ufaransa kufunga 2, hivyo kutawazwa kuwa mabingwa wa Kombe la Dunia la Fifa 2022.

Klian Mbappe ametangazwa kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo baada ya kufunga jumla ya magoli manane. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha