Xi Jinping akutana na Medvedev, Mwenyekiti wa Chama Tawala cha Russia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 22, 2022
Xi Jinping akutana na Medvedev, Mwenyekiti wa Chama Tawala cha Russia
Xi Jinping, Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Rais wa China, akisalimiana na Dmitry Medvedev Mwenyekiti wa chama tawala cha Russia cha United Russia, ambaye anazuru China kutokana na mwaliko wa CPC, katika Jumba la Wageni la Diaoyutai hapa Beijing, China, Desemba 21, 2022. (Xinhua/Liu Weibing)

BEIJING - Xi Jinping, Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Rais wa China, Jumatano alikutana na Dmitry Medvedev Mwenyekiti wa chama tawala cha Russia cha United Russia, ambaye anatembelea China kutokana na mwaliko wa CPC.

Huku akimwomba Medvedev kuwasilisha salamu njema na za heri kwa Rais wa Russia Vladimir Putin, Xi amesema Mkutano Mkuu wa 20 wa CPC umeweka wazi kazi kuu za kujenga nchi kubwa ya kijamaa yenye maendeleo ya kisasa kwa pande zote na kuendeleza ustawishaji wa Taifa la China katika sekta zote kupitia njia ya Maendeleo ya Kisasa ya China.

China ina imani kamili ya kufuata njia ya maendeleo ya kisasa ya China na kutoa fursa zaidi kwa amani na ustawi wa Dunia, amesema Rais Xi.

Rais Xi ameongeza kuwa mfumo wa mazungumzo kati ya CPC na chama cha United Russia kwa muda mrefu umekuwa njia na jukwaa la kipekee kwa nchi hizo mbili ili kuimarisha hali ya kuaminiana kisiasa, kuhimiza ushirikiano wa kunufaishana, na kuonyesha uratibu wa kimkakati, na mambo haya yanaunga mkono maendeleo thabiti ya uhusiano wa pande mbili katika zama mpya.

Huku akiweka bayana kuwa mabadilishano ya sasa kati ya pande hizo mbili yameingia katika muongo wa tatu, Rais Xi amesema pande hizo mbili zitaendelea kuwa na majadiliano ya kina kuhusu uzoefu wa utawala, kuunganisha mikakati ya maendeleo, na kuhimiza ushirikiano wa kimataifa na wa pande nyingi kati ya vyama vya siasa. Xi ametumai vyama viwili vinaweza kufundishana katika kujenga vyama tawala na kuchangia hekima na nguvu ili kuimarisha uratibu wa kimkakati wa China na Russia.

Rais Xi amesema China iko tayari kushirikiana na Russia kusukuma mbele uhusiano kati ya China na Russia katika zama mpya na kufanya utawala wa kimataifa kuwa wenye haki na usawa.

Kuhusu mgogoro wa Ukraine, China inaamua msimamo na sera yake kwa kuzingatia hali halisi ya jambo husika, inashikilia ukweli na usawa, na kuhimiza kikamilifu mazungumzo ya amani, Xi amesema. Tunatumai, pande zinazohusika zitaendelea kuwa na busara na kujizuia, kufanya mazungumzo ya kina, na kushughulikia masuala ya pamoja ya usalama kupitia njia za kisiasa.

Medvedev amemkabidhi Rais Xi barua kutoka kwa Rais Putin, akiwasilisha salamu za kirafiki na salamu za heri kwa Rais Xi. Pia ametoa pongezi za dhati kwa Rais Xi kwa kuchaguliwa tena kuwa Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya CPC na kwa matokeo ya Mkutano Mkuu wa 20 wa CPC.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha