

Lugha Nyingine
Barabara Kuu ya Nairobi iliyojengwa na China yafikisha watumiaji milioni 10 (4)
NAIROBI - Kampuni ya Moja Expressway inayosimamia na kuendesha Barabara Kuu ya Nairobi yenye urefu wa kilomita 27.1, iliyojengwa na kampuni ya China chini ya ushirikiano wa ubia kati ya serikali na kampuni binafsi siku ya Jumanne imewashukuru madereva wa magari milioni kumi ambao wameitumia tangu kuzinduliwa kwake rasmi Julai 2022.
Maofisa wakuu, watendaji wakuu na madereva wa kawaida wa magari walipamba hafla hiyo kuadhimisha kufikia watumiaji milioni kumi kwenye barabara hiyo ya kisasa ambayo imerahisisha usafiri na usafirishaji bidhaa kutoka upande wa kusini wa mji mkuu wa Kenya, Nairobi ambako uwanja mkuu wa ndege unapatikana, hadi wilaya kuu ya Westlands.
Joseph Mbugua, Katibu Mkuu wa Idara ya Miundombinu ameuzungumzia mradi huo wa Barabara Kuu ya Nairobi kuwa kihistoria ambao umeimarisha usafirishaji wa watu na mizigo, na kuifanya nchi hiyo kuwa kitovu cha kibiashara na ugavi.
Ameongeza kuwa kwa mchango wa barabara hiyo, utalii wa mikutano umepata mng'ao na kuongeza kuwa uhusiano wake na uwanja mkuu wa ndege, Reli ya Kisasa ya Mombasa-Nairobi (SGR) iliyojengwa na China na barabara nyingi za mzunguko katika mji mkuu umeboresha tija ya uchumi wa nchi hiyo kwa ujumla.
Barabara Kuu ya Nairobi ni barabara kuu ya Daraja la A yenye barabara mbili zinazokwenda sambamba za kupitisha magari katika njia nne, kila moja ambazo huwa na njia sita katika baadhi ya sehemu huku ikiwa na njia 15 za kuingia na 14 za kutokea ili kuwahakikishia madereva mwendo usio wa mashaka kuelekea maeneo mbalimbali.
Ujenzi wa Barabara Kuu ya Nairobi uliofanywa na Shirika la China la Barabara na Madaraja ulianza Septemba 2020 na matumizi yake kwa majaribio yalianza Mei 2022, na hivyo kufungua njia ya kuzinduliwa kwake rasmi na Rais wa Kenya wa wakati huo, Uhuru Kenyatta mnamo Julai 31, 2022.
Steve Zhao, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Moja Expressway ambayo iinafanya usimamizi na matengenezo ya barabara hiyo, amesema kuwa kwa wastani, madereva 50,000 walikuwa wakitumia kila siku, kutoka 10,000 katika robo ya mwisho ya Mwaka 2022.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma