Wanafunzi wa Kimataifa waanza kurudi China kwa furaha na matumaini

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 28, 2023
Wanafunzi wa Kimataifa waanza kurudi China kwa furaha na matumaini
Mwanafunzi kutoka Indonesia Joshua Timothy Solomon (wa kwanza kulia, nyuma) akiwa pamoja na wanafunzi wengine wa Indonesia huko Guangzhou, Mkoa wa Guangdong, Kusini mwa China, Januari 15, 2023. (Xinhua)

TAIYUAN/GUANGZHOU - Wakati Alansi Mohammed alipoona eneo la Uwanda mkubwa wa udongo manjano kupitia dirisha dogo tena, alipata msisimko kiasi kwamba moyo wake karibu "kuruka."

"Imekuwa ni miaka mitatu. Hatimaye nimefanikiwa kurejea katika mji wangu wa pili wa nyumbani (China)," amesema raia huyo wa Yemen.

Alansi ni mwanafunzi anayesomea fani ya biashara ya kielektroniki katika Chuo Kikuu cha Shanxi katika Mji wa Taiyuan, mji mkuu wa Mkoa wa Shanxi, Kaskazini mwa China. Alirudi nyumbani kwa ajili ya likizo ya msimu wa baridi Januari 2020.

China iliondoa kwa kiasi kikubwa masharti ya usimamizi wake wa UVIKO-19 na kuwezesha usafiri rahisi na wa utaratibu wa kuvuka mpaka kwa Wachina na raia wa kigeni mapema Januari 2023. Muhula mpya wa masomo unapokaribia, wanafunzi wengi wa kimataifa kama Alansi wanamiminika kurudi China ili kuanza tena maisha ya chuo kikuu kwa msisimko na matumaini.

Takwimu kutoka Wizara ya Elimu ya China zinaonyesha kuwa karibu wanafunzi 500,000 wa kigeni kutoka nchi na maeneo 196 walikuwa wakisoma nchini China Mwaka 2018. Kwa miaka mitatu iliyopita, wale ambao walikuwa wamerejea katika nchi zao walilazimika kuchukua masomo mtandaoni ili kuendelea na masomo.

"Baada ya kufahamishwa kuwa naweza kurudi, chuo changu kilitoa msaada wa pande zote, huku utaratibu wa kuingia nchini China umekuwa rahisi, na hivyo safari nzima ilikuwa safi," amesema Alansi, ambaye anaamini marekebisho ya China ya sera za kutoka na kuingia nchini China yanaweza kuhimiza sana kurejea kwa mabadilishano ya watu duniani, na ameongeza kuwa yeye ni mmoja wa wafaidika.

Ili kukaribisha idadi kubwa ya wanafunzi wa kimataifa wanaorejea, vyuo vikuu vingi vimeanza kutoa huduma zinazofaa zikilenga kurahisisha kurejea kwa wanafunzi vyuoni na kuwapa huduma stahiki.

"Kama nilivyotarajia, China bado imejaa nguvu na pilikapilika nyingi. Inaonekana kama sikuwahi kuondoka," amesema Dania Zaman Dania mwanafunzi wa kigeni anayesoma masomo ya tiba za binadamu katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Shaanxi, Mkoa wa Shaanxi, China.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha