

Lugha Nyingine
Shirika lisilo la kiserikali la China lasaidia wagonjwa kurejesha uwezo wa kuona kupitia upasuaji wa mtoto wa jicho nchini Djibouti
DJIBOUTI CITY - GX Foundation, shirika lisilo la faida na lisilo la kiserikali lililosajiliwa Hong Kong, China, Jumatatu limeanzisha rasmi mradi unaolenga kutoa huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho kwa wagonjwa na kuwasaidia kurejesha uwezo wa kuona katika nchi ya Djibouti ya Bahari Nyekundu.
Shirika hilo limehuisha mkataba wake wa maelewano na Wizara ya Afya ya Djibouti ili kuendeleza ushirikiano wao hadi Mwaka 2027, ambapo chini ya utekelezaji wake watu zaidi ya 6000 watafanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho utakaofanywa bure kwa wagonjwa wenyeji katika miaka michache ijayo.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi huo, Leung Chun-ying, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la Umma la China na Mwenyekiti wa shirika hilo, amesema shirika hilo linatarajia kutumia mradi huo wa kutokomeza upofu unaotokana na mtoto wa jicho ili kuonesha kikamilifu mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya China (NGO) katika msaada wa kimataifa wa kibinadamu.
Katika hotuba yake, Waziri wa Afya wa Djibouti Ahmed Robleh Abdilleh ametoa pongezi kwa ushirikiano mzuri kati ya Djibouti na China katika sekta ya afya.
Abdilleh amesema mtoto wa jicho ni moja ya sababu kuu za upofu nchini Djibouti na kuwa na athari kubwa katika maendeleo ya jamii na uchumi. Ameshukuru kwa msaada huo wa msingi, akisema kwamba sasa Djibouti inaweza kufanya shughuli mbalimbali za utafiti wa mtoto wa jicho na upasuaji ili kupunguza upofu kwa kiasi kikubwa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma