Mkutano wa Pili wa Wajumbe wote wa Kamati Kuu ya 20 ya CPC watoa taarifa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 01, 2023
Mkutano wa Pili wa Wajumbe wote wa Kamati Kuu ya 20 ya CPC watoa taarifa
Xi Jinping, Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) akitoa hotuba muhimu kwenye Mkutano wa Pili wa Wajumbe wote wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China hapa Beijing, Mji Mkuu wa China. Mkutano huo wa wajumbe wote umefanyika kuanzia Februari 26 hadi 28, 2023. (Xinhua/Ju Peng)

BEIJING - Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) imetoa taarifa baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Pili wa wajumbe wote siku ya Jumanne.

Xi Jinping, Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, alitoa hotuba muhimu kwenye mkutano huo uliofanyika kwa siku tatu na kuongozwa na Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China.

Kwenye mkutano huo, Kamati Kuu ya CPC ilisikiliza na kujadili ripoti ya kazi iliyowasilishwa na Xi akiwa kwa niaba ya Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya CPC.

Mkutano huo umepitisha orodha ya maofisa wanaopendekezwa kushika nafasi za uongozi wa vyombo vya serikali itakayowasilishwa kwenye Mkutano wa Kwanza wa Bunge la Umma la 14 la China (NPC) ili ithibitishwe. Mkutano pia umepitisha orodha ya maofisa viongozi wanaopendekezwa wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la Umma la China ili ithibitishwe kwenye Mkutano wa Kwanza wa Baraza la 14 la Mashauriano ya Kisiasa la umma la China.

Mkutano huo pia umepitisha mpango wa mageuzi ya vyombo vya Chama na serikali ambao utawasilishwa kwenye Bunge la Umma la 14 la China ili kuthibitishwa. Kabla ya kupitishwa kwake, Xi alitoa maelezo ya ufafanuzi juu ya rasimu ya mpango huo kwenye mkutano.

Mkutano huo pia umesisitiza kuwa mikutano ijayo ya Bunge la Umma na Baraza la Mashauriano ya Kisiasa ina umuhimu mkubwa katika kuhamasisha zaidi Chama kizima na watu wa makabila yote ya China kujitahidi kwa mshikamano kujenga nchi ya kijamaa yenye maendeleo ya kisasa kwa pande zote na kuendeleza ustawishaji mkubwa wa Taifa la China kwa pande zote.

Mkutano umetambua kwamba tangu Mkutano Mkuu wa 18 wa CPC, Kamati Kuu ya CPC chini ya uongozi wa Komredi Xi Jinping imeichukulia kazi ya kuendeleza kwa kina mageuzi ya vyombo vya Chama na serikali kuwa jukumu muhimu katika kuufanya mfumo na uongozi wa China kuwa wa kisasa.

Mkutano umesisitiza kuwa juhudi zinahitajika ili kuongeza mageuzi ya vyombo katika maeneo muhimu na kuhakikisha kwamba uongozi wa Chama juu ya maendeleo ya kijamaa unakuwa bora zaidi katika mpangilio wa mifumo, kuimarika zaidi katika mgawanyo wa majukumu, kukamilisha mifumo na taratibu, na kuongeza ufanisi zaidi katika uendeshaji na usimamizi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha