Kimbunga Freddy chaua zaidi ya watu 200 Kusini mwa Afrika (6)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 16, 2023
Kimbunga Freddy chaua zaidi ya watu 200 Kusini mwa Afrika
Mvulana akiwa ameketi kwenye nyumba iliyobomolewa huko Blantyre, Malawi, Machi 14, 2023. (Picha na Joseph Mizere/Xinhua)

BLANTYRE/MAPUTO - Kimbunga Freddy kimeendelea kusababisha uharibifu katika eneo la Kusini mwa Afrika huku idadi ya vifo kutokana na majanga kama vile mafuriko na maporomoko ya udongo ikiendelea kuongezeka.

Nchini Malawi, ambako athari za kimbunga hicho zinaonekana kuwa kali zaidi, idadi ya watu waliofariki imeongezeka hadi 190 huku miili zaidi ikipatikana Jumanne kufuatia uharibifu uliosababishwa na kimbunga Freddy cha kitropiki, ambacho sasa kimeathiri wilaya na miji 12 katika nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika.

Idara ya Kukabiliana na Majanga nchini Malawi (DoDMA) imesema hayo kwenye taarifa yake mpya ya Jumanne alasiri, huku kamishna Charles Kalemba akisema watu 158 wamefariki katika Mji wa Blantyre pekee, mji wa kibiashara wa nchi hiyo.

Kimbunga hicho cha kitropiki kilianza kuikumba Malawi Jumatatu baada ya kuingia katika Jimbo la Zambezia nchini Msumbiji Ijumaa, na kusababisha mafuriko, maporomoko ya matope na uharibifu uliosababishwa na upepo mkali katika wilaya na miji 12 ya Malawi.

Kwa mujibu wa DoDMA, katika nchi nzima ya Malawi watu 584 wamejeruhiwa na watu 37 hawajulikani walipo, wakiwemo askari watatu wa kikosi cha uokoaji baada ya boti yao kugonga mti na kupinduka. Ripoti hiyo mpya pia imesema takriban watu 58,946 wameathiriwa, na takriban watu 19,371 kati yao wameyahama makazi yao.

Rais Lazarus Chakwera alikatisha ziara yake nchini Afrika Kusini ambako alikuwa akizuru baada ya kutoka kwenye Mkutano wa 5 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Nchi zilizoko nyuma zaidi kimaendeleo mjini Doha, Qatar, na kurejea Malawi Jumanne.

Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kamuzu Banda, kiongozi huyo wa Malawi alielezea athari za Kimbunga Freddy kuwa za kusikitisha na kusema kwamba atatembelea maeneo na watu walioathirika.

Nchini Msumbiji, jirani wa Malawi, takriban watu 10 pia wamefariki dunia na wengine 13 kujeruhiwa wakati wa kupita kwa mara ya pili kwa kimbunga hicho, amesema ofisa kutoka Taasisi ya Kitaifa ya Kudhibiti na Kupunguza Hatari (INGD) siku ya Jumanne.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha