Waziri Mkuu wa China asisitiza kuendeleza viwanda vinavyotumia teknolojia za hali ya juu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 23, 2023
Waziri Mkuu wa China asisitiza kuendeleza viwanda vinavyotumia teknolojia za hali ya juu
Waziri Mkuu wa China Li Qiang, ambaye pia ni Mjumbe wa Kudumu wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, akitembelea Kampuni ya Teknolojia ya Lens huko Changsha, Mkoa wa Hunan, Katikati mwa China, Machi 22, 2023. Waziri Mkuu Li amefanya ziara ya ukaguzi na kuongoza kongamano la maendeleo ya viwanda vinavyotumia teknolojia za hali ya juu katika Mkoa wa Hunan, China kuanzia Jumanne hadi Jumatano. (Xinhua/Rao Aimin)

CHANGSHA - Waziri Mkuu wa China Li Qiang amehimiza juhudi za kuyapa kipaumbele cha juu maendeleo yenye ubora wa juu, kutilia mkazo maendeleo ya uchumi halisi, kuweka msukumo mkubwa wa kuendeleza viwanda vinavyotumia teknolojia za hali ya juu, bidhaa za viwandani zenye ubora wa juu, na kuongeza kasi katika ujenzi wa mfumo wa kisasa wa viwanda.

Li, ambaye pia ni Mjumbe wa Kudumu wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China alihimiza hayo alipofanya ziara ya ukaguzi na kwenye kongamano la maendeleo ya viwanda vinavyotumia teknolojia za hali ya juu katika Mkoa wa Hunan uliopo katikati mwa China kuanzia Jumanne hadi Jumatano.

Kwenye ziara zake katika kampuni mbalimbali za biashara za Zhuzhou, ikiwa ni pamoja na Kampuni ya CRRC Zhuzhou Locomotive, Waziri Mkuu Li alifahamishwa kwa undani kuhusu uzalishaji, utafiti na maendeleo, na uendelezaji wa masoko ya kampuni hizo.

Amesema kukuza maendeleo ya viwanda vinavyotumia teknolojia za hali ya juu kimsingi kunategemea uvumbuzi na talanta. Amesema, kampuni zinapaswa kuharakisha kufikia mafanikio katika teknolojia za msingi katika sekta muhimu na katika teknolojia na vifaa muhimu.

Waziri Mkuu Li amesema, thamani na uhai wa uvumbuzi wa kiteknolojia upo katika matumizi yake. Amehimiza ushirikiano zaidi kati ya viwanda, wasomi, utafiti na matumizi yake, na kutaka kuinuliwa kwa kiwango na ubora wa bidhaa.

Wakati akiongoza kongamano la maendeleo ya sekta ya viwanda vinavyotumia teknolojia za hali ya juu, Waziri Mkuu Li amesema kuwa uchumi halisi, hasa sekta ya viwanda, ndiyo msingi wa uchumi wa China.

"Mazingira ya biashara yenye mwelekeo wa soko, yanayofuata msingi wa sheria na ya kimataifa yanapaswa kuundwa, na mwelekeo wa sera kusaidia sekta ya viwanda vinavyotumia teknolojia ya hali ya juu unapaswa kuimarishwa," amesema.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha