

Lugha Nyingine
Mji wa New York, Marekani waimarisha hatua za usalama huku kukiwa na sintofahamu juu ya kesi ya Trump
![]() |
Polisi wakilinda mbele ya jengo la Trump Tower mjini New York, Marekani, Machi 21, 2023. (Xinhua/Liu Yanan) |
NEW YORK - Vyombo vya kusimamia utekelezaji wa sheria katika Jiji la New York, Marekani vimeimarisha hatua za usalama katika maeneo nyeti baada ya Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kudokeza hivi karibuni kwamba atakamatwa Jumanne (kwa saa za huko) na kuwataka wafuasi wake kufanya maandamano.
Idara ya Polisi ya New York imeweka vizuizi vingi na kupeleka polisi karibu na Mahakama ya Jinai ya Manhattan na Ofisi ya Mwanasheria wa Wilaya ya Manhattan huko Lower Manhattan, New York na vile vile kwenye jengo la Trump Tower liliko Fifth Avenue huko Midtown, New York.
Hadi wakati Shirika la Habari la China Xinhua linaripoti habari hii, hakukuwa na umati mkubwa ulioonekana katika Jiji la New York licha ya uwepo wa waandishi wengi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari kwenye maeneo hayo.
Hakukuwa na taarifa zozote za kushtakiwa kwa Trump kutoka Ofisi ya Mwanasheria wa Wilaya ya Manhattan hadi kufikia Jumanne alasiri kwa saa za huko.
Ofisi ya Mwanasheria wa Wilaya ya Manhattan inachunguza ikiwa Trump alighushi nyaraka zenye rekodi za biashara kuhusiana na madai ya malipo ya kimyakimya yaliyofanywa kwa nyota wa filamu za watu wazima wakati wa kampeni za urais Mwaka 2016, kwa mujibu wa habari zilizochapishwa na kuripotiwa na vyombo vya habari.
Ofisi ya Mwanasheria wa Wilaya ya Manhattan imekataa kuthibitisha au kutoa maoni yake iwapo Trump atafunguliwa mashtaka au laa, ikisema "haitatishwa na majaribio ya kuhujumu mchakato wa haki."
Novemba 2022, Trump alitangaza azma yake ya kugombea tena urais katika uchaguzi wa rais wa Mwaka 2024 huku muda wake wa kwanza wa urais ukikamilika Januari 2021 baada ya kushindwa na Rais wa sasa Joe Biden kwenye uchaguzi wa Mwaka 2020.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma